Mwanzo Utangulizi

Utangulizi
Neno “Mwanzo” linatokana na neno la Kiyunani “Geneseos” ambalo maana yake ni “Asili,” “Chimbuko,” au “Chanzo”; linatokana na tafsiri ya Agano la Kale ya Kiyunani ijulikanayo kama “Septuagint.” Kitabu hiki kinaeleza mwanzo wa ulimwengu, mwanzo wa mwanadamu (yaani mwanamke na mwanaume), mwanzo wa dhambi ya mwanadamu, mwanzo wa ahadi na mpango wa Mungu wa wokovu, na uhusiano wa kipekee kati ya Abrahamu na Mungu. Pia kinaeleza juu ya watu mahsusi wa Mungu, na mipango yake katika maisha yao. Baadhi ya watu hawa ni Adamu na Eva, Noa, Abrahamu, Isaki, Yakobo, Yosefu na ndugu zake, na wengine wengi.
Mwanzo ni kitabu cha kwanza miongoni mwa vitabu vinavyoitwa “Vitabu Vitano vya Mose” vilivyoko mwanzoni mwa Biblia. Vitabu hivi vinaitwa pia Vitabu vya Sheria kwa sababu ndipo palipoandikwa maagizo na sheria za Mungu kwa watu wa Israeli. Kitabu cha Mwanzo kama kitabu cha utangulizi kinaelezea habari za Mungu kwanza, na kuendelea kujifunua mwenyewe kwa wanadamu, ambalo ni jambo la muhimu sana. Katika kitabu hiki tunapata ahadi ya kwanza kabisa ya ukombozi wa mwanadamu aliyeanguka: “…uzao wa mwanamke utakuponda kichwa…” (3:15). Kitabu cha Mwanzo kinaelezea jinsi ilivyotokea hadi Israeli wakafanyika watu maalum wa Mungu.
Mwandishi
Wayahudi na Wakristo wanashikilia mwandishi ni Mose.
Kusudi
Kumfunulia mwanadamu mwanzo wa kuumbwa kwa mbingu na nchi, na vyote vilivyomo. Kumwonyesha kuwa Mungu ndiye Muumbaji pekee.
Mahali
Katika Ghuba ya Sinai, watu wa Israeli walipokuwa jangwani.
Tarehe
Kati ya 1450–1410 K.K.
Wahusika Wakuu
Adamu, Eva, Noa, Abrahamu, Sara, Isaki, Rebeka, Yakobo, Yosefu.
Wazo Kuu
Kueleza uumbaji, kuanguka kwa mwanadamu, na ahadi ya ukombozi wa mwanadamu kwa njia ya Yesu Kristo. Kila msingi mkuu wa imani katika Maandiko una mizizi yake katika Mwanzo kama asili, kitu kamili, au mfano, au ufunuo halisi.
Mambo Muhimu
Uumbaji, kuanguka kwa mwanadamu, ahadi za ukombozi wa mwanadamu kupitia Yesu Kristo.
Mgawanyo
Kuumbwa kwa ulimwengu, na mwanadamu (1:1–2:25)
Kuanguka kwa mwanadamu na matokeo ya dhambi (3:1–5:32)
Habari za Noa (6:1–9:29)
Kutawanywa kwa mataifa (10:1–11:32)
Maisha ya Abrahamu (12:1–25:18)
Isaki na familia yake (25:19–26:35)
Yakobo na wanawe (27:1–37:1)
Maisha ya Yosefu (37:2–50:26).

Kleurmerk

Deel

Kopieer

None

Wil jy jou kleurmerke oor al jou toestelle gestoor hê? Teken in of teken aan