Mordekai aliandika matukio haya, naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote walioko katika majimbo ya Mfalme Ahasuero, majimbo yaliyo mbali na karibu, akiwataka kila mwaka washerehekee siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari kama wakati ambao Wayahudi walipata nafuu kutoka kwa adui zao na kama mwezi ambao huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha na kuomboleza kwao kuwa siku ya kusherehekea. Aliwaandikia kushika siku hizo kama siku za karamu na za furaha na kupeana zawadi za vyakula wao kwa wao na zawadi kwa maskini.