Utangulizi
Kumbukumbu la Torati limetokana na neno la Kiyunani “Deuteronomion” ambalo maana yake ni “Kutolewa kwa amri mara ya pili.” Kitabu hiki kilipewa jina hili na watafsiri wa Agano la Kale, yaani “Septuagint” kwa Kiyunani. Kitabu hiki ndicho cha mwisho katika ule mgawanyo wa kwanza wa Agano la Kale ambao huitwa “Vitabu Vitano vya Sheria.” Katika hotuba zilizonakiliwa katika Kumbukumbu la Torati, Mose anafanya ufupisho wa dini ya Waisraeli kuwa Agano lililotolewa kwa baba zao. Hili Agano ndilo msingi wa uhusiano ulioanzishwa na Mungu baina yake na Waisraeli, wala si Sheria, ambayo sasa inadhihirishwa kwa Waisraeli kwa kuokolewa kutoka Misri na kutunzwa kwa muda wote wa kutangatanga huko jangwani. Baada ya miaka arobaini, Waisraeli walikuwa wamekaribia kuingia katika Nchi ya Ahadi. Lakini kabla ya kufanya hivyo, Mose alitaka kuwakumbusha historia yao, yaani, yale yote ambayo Mungu alikuwa amewatendea, pamoja na amri zile zote walizopaswa kuendelea kutii kama taifa teule la Mungu.
Mazungumzo ya kwanza ya Mose yalikuwa kuwakumbusha watu kuhusu wema wa Mungu kwa kipindi chote cha safari ili kuwapa nchi ya Kanaani. Mazungumzo ya pili yalikuwa ni muhtasari wa Sheria za Mungu zikiwepo Amri Kumi. Mose aliwaambia watu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa nguvu zako zote” (6:5) ili waweze kuendelea kuzifurahia baraka za Mungu. Pia Mose alitilia mkazo ukweli kwamba ili waweze kuwa na uhusiano mzuri na Mungu, ilikuwa ni lazima watu wawafundishe watoto wao kumpenda Mungu na kuzitii amri zake. Kutokana na hilo, haki na uadilifu zingepenya katika maisha yao ya kila siku, kadiri ambavyo upendo wao ungeelekezwa kwa ndugu wa kiume na wa kike.
Mwandishi
Mose aliandika kitabu hiki, isipokuwa sura inayoeleza kuhusu kifo chake.
Kusudi
Kusudi kubwa lilikuwa kuwakumbusha Waisraeli juu ya mambo yale ambayo Mungu alikuwa amewatendea, na kuwahimiza wajitoe kwake.
Mahali
Mashariki mwa Mto Yordani, karibu na Yeriko, wakiwa wanaikabili nchi ya Kanaani.
Tarehe
Kati ya 1407–1406 K.K.
Wahusika Wakuu
Mose na Yoshua.
Wazo Kuu
Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kinaishia kwa kuwakumbusha Waisraeli juu ya Agano ambalo Mungu alifanya nao (29), kuteuliwa kwa Yoshua kuwa kiongozi mpya (31), na kifo cha Mose (34).
Mambo Muhimu
Ili kudumisha uhusiano wa upendo kati ya Waisraeli na Mungu, wazazi waliagizwa kuwafundisha watoto wao kumcha Mungu kwa kuwafundisha kwa kielelezo (4:9-10; 6:7). Kwa njia ya kuadhimisha zile sikukuu za mwaka, yaani Pasaka, Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, Sikukuu ya Vibanda, Sikukuu ya Mavuno, pamoja na yale makusanyiko mengine, Waisraeli walivikumbusha vizazi vilivyofuata juu ya upendo wa Mungu ulioonyeshwa kwenye ukombozi wao kutolewa Misri na kuendelea kwao kutunzwa naye kwa kuwapa mazao.
Mgawanyo
Mazungumzo ya kwanza ya Mose (1:1–4:43)
Mazungumzo ya pili ya Mose (4:44–11:32)
Sheria za maisha ya kila siku (12:1–26:19)
Matokeo ya kutii na kutokutii (27:1–28:68)
Kufanya upya Agano (29:1–30:20)
Baraka za Mose kwa Israeli, na kifo cha Mose (31:1–34:12).