YouVersion Logo
Search Icon

Mhubiri 10

10
1 Kama vile nzi waliokufa huacha harufu mbaya kwenye manukato,
ndivyo upumbavu kidogo huzidi nguvu hekima na heshima.
2Moyo wa mwenye hekima huelekea kuume,
lakini moyo wa mpumbavu huelekea kushoto.
3Hata anapotembea barabarani,
mpumbavu hukosa ufahamu
na kudhihirisha kwa kila mmoja
jinsi alivyo mpumbavu.
4 Kama hasira ya mtawala ikiwaka dhidi yako,
usiache mahali pako,
utulivu huweza kuzuia makosa mengi.
5Kuna ubaya niliouona chini ya jua,
aina ya kosa litokalo kwa mtawala:
6 Wapumbavu kuwekwa kwenye nafasi nyingi za juu,
wakati matajiri hushika nafasi za chini.
7 Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi,
wakati wakuu wakitembea
kwa miguu kama watumwa.
8 Yeye achimbaye shimo
aweza kutumbukia ndani yake,
yeyote abomoaye ukuta
anaweza kuumwa na nyoka.
9 Yeyote apasuaye mawe
inawezekana yakamuumiza,
yeyote apasuaye magogo
inawezekana yakamuumiza.
10Kama shoka ni butu
na halikunolewa,
nguvu nyingi zinahitajika,
lakini ustadi utaleta mafanikio.
11 Kama nyoka akiuma kabla ya kufanyiwa uaguzi,
mwaguzi hatahitajika tena.
12 Maneno yatokayo kinywani mwa mtu mwenye hekima
yana neema,
bali mpumbavu huangamizwa
na midomo yake mwenyewe.
13Mwanzoni maneno yake ni upumbavu,
mwishoni ni wazimu mbaya,
14 naye mpumbavu huzidisha maneno.
Hakuna yeyote ajuaye linalokuja,
ni nani awezaye kueleza ni jambo gani
litakalotokea baada yake?
15Kazi ya mpumbavu humchosha mwenyewe,
hajui njia iendayo mjini.
16 Ole wako, ee nchi ambayo mfalme wako alikuwa mtumwa
na ambayo wakuu wako hufanya karamu asubuhi.
17 Heri wewe, ee nchi ambayo mfalme wako ni wa uzao wenye kuheshimika
na ambayo wakuu wako hula chakula kwa wakati unaofaa:
ili kupata nguvu na si kwa ajili ya ulevi.
18 Kama mtu ni mvivu paa la nyumba huinama,
kutokana na mikono milegevu, nyumba huvuja.
19 Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko,
nao mvinyo hufurahisha maisha,
lakini fedha ni jawabu la mambo yote.
20 Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako,
au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala,
kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako,
naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema.

Currently Selected:

Mhubiri 10: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in