Utangulizi
Neno “Kutoka” linatokana na neno la Kiyunani “Exodos”, ambalo maana yake ni “Kutoka”, “Kuhama” au “Kuondoka”; jina hili lilipewa kitabu hiki na watafsiri wa Agano la Kale la Kiyunani lijulikanalo kama “Septuagint.” Kitabu hiki kinatokana na maajabu makubwa aliyoyafanya Mungu katika uhusiano wake na watu wake wa Israeli kwa kuwaondoa utumwani huko nchi ya Misri. Huu ni muujiza mkubwa katika historia ya Waisraeli.
Kutokana na hali hiyo, Mungu alimchagua Mose kwa kazi maalum ya kuwaokoa Waisraeli kutoka utumwani Misri, kuwaongoza na kuwapeleka nchi ya Kanaani, ambayo Mungu alikuwa amewaahidi baba zao.
Mungu alionyesha nguvu zake kwa Waisraeli na kwa Wamisri katika yale mapigo kumi. Pigo la mwisho lilisababisha Waisraeli waruhusiwe kuondoka Misri. Kabla ya Waisraeli kuondoka Misri waliadhimisha Sikukuu ya Pasaka. Tukio hili lilifanyika katika historia iliyofuata baadaye na kuandikwa katika vitabu vya Israeli.
Waisraeli walianza safari yao wakiwa wanalindwa na kuongozwa na Mungu katika nguzo ya wingu wakati wa mchana, na nguzo ya moto wakati wa usiku. Waisraeli walipofika Mlima Sinai, hapo ndipo Mungu alipofanya Agano lake na Waisraeli na kuwapa sheria za kuwaongoza jinsi watakavyoishi na kumwabudu, kwani hapo ndipo Mose alipopewa ufunuo mkuu wa Mungu akipewa kiini na asili ya dini ya Kiyahudi.
Mwandishi
Mose.
Kusudi
Kuelezea matukio yaliyotokea katika ukombozi wa watu wa Israeli katika nchi ya Misri na vile waliendelea hadi kuwa taifa.
Mahali
Wakati Waisraeli walikuwa jangwani, mahali fulani katika Ghuba ya Sinai.
Tarehe
Miaka ya 1450–1410 K.K., wakati mmoja na kitabu cha Mwanzo.
Wahusika Wakuu
Mose, Aroni, Miriamu, Farao, Binti Farao, Yethro, Yoshua na Bezaleli.
Wazo Kuu
Kitabu cha Kutoka kinaelezea vile Waisraeli waliteswa na kugandamizwa wakati walikuwa utumwani katika nchi ya Misri, kukombolewa kwao kwa uwezo wa Mungu, kufanyika kwa Agano kati yao na Mungu, kupewa Sheria, kujengwa kwa Hema, na mwanzo wa ukuhani wa Aroni.
Mambo Muhimu
Kutolewa utumwani, na kuanzishwa kwa Pasaka; kuongozwa na Mungu, na kuingia kwenye Agano na Mungu; kuanzishwa kwa uhusiano baina ya Israeli na Mungu; na Israeli kutambuliwa kuwa taifa takatifu la Mungu, kwa njia ya kumwabudu Mungu kwa moyo wote na kumtii.
Mgawanyo
Mose, kiongozi aliyechaguliwa na Mungu (1:1–4:31)
Ugumu wa Farao na matokeo yake (5:1–11:10)
Kuanzishwa kwa Pasaka na pigo la mwisho (12:1-30)
Kutoka Misri hadi Mlima Sinai (12:31–19:2)
Agano la Mungu na amri zake (19:3–24:8)
Hema ya ibada (24:9–40:38).