6
Kuwapa wahitaji
1“Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.
2“Hivyo mnapowapa wahitaji, msitangaze hadharani kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi#6:2 Nyumba za ibada na mafunzo. na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.
Kuhusu maombi
(Luka 11:2-8)
5“Nanyi mnaposali, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 6Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. 7Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. 8Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.
9“Hivi ndivyo mnavyopaswa kuomba:
“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe.
10Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.
11Utupatie riziki yetu
ya kila siku.
12Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tulivyokwisha
kuwasamehe wadeni wetu.
13Usitutie majaribuni,
bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu
[kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu,
na utukufu, hata milele. Amen]#6:13 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya..’
14Kwa kuwa mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
Kuhusu kufunga
16“Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao kamilifu. 17Lakini unapofunga, jipake mafuta kichwani na kunawa uso wako, 18ili kufunga kwako kusionekane na watu wengine ila Baba yako anayeketi mahali pa siri; naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako kwa wazi.
Kuweka hazina mbinguni
(Luka 12:33-34)
19“Msijiwekee hazina duniani, ambapo nondo na kutu huharibu, nao wezi huvunja na kuiba. 20Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wezi hawavunji na kuiba. 21Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.
Taa ya mwili
(Luka 11:34-36)
22“Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. 23Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Hivyo basi, ikiwa nuru iliyo ndani yako ni giza, je, hilo ni giza nene aje!
Kutumikia Mwenyezi Mungu na mali
(Luka 16:13; 12:22-31)
24“Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali#6:24 au Utajiri; yaani Mamoni kwa Kiaramu au Mamona kwa Kiyunani.
Msiwe na wasiwasi
(Luka 12:22-31)
25“Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? 26Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani kuliko hao ndege? 27Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?
28“Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29Lakini nawaambia, hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33Lakini utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Kila siku ina masumbufu yake ya kutosha.