13
Dalili Za Siku Za Mwisho
(Mathayo 24:1-2; Luka 21:5-6)
1 Yesu alipokuwa akitoka Hekaluni, mmojawapo wa wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu! Tazama jinsi mawe haya yalivyo makubwa, na majengo haya yalivyo mazuri!”
2 Ndipo Yesu akajibu akasema, “Je, unayaona majengo haya yalivyo makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali yote yatabomolewa.”
Mateso Yatabiriwa
(Mathayo 24:3-14; Luka 21:7-19)
3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni mkabala na Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamuuliza faraghani, 4 “Tafadhali tuambie, mambo haya yatatukia lini? Nayo dalili ya kuwa hayo yote yanakaribia kutimia itakuwa gani?”
5 Yesu akawaambia: “Jihadharini mtu yeyote asiwadanganye. 6Wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye,’ nao watawadanganya wengi. 7Msikiapo habari za vita na uvumi wa vita, msiwe na hofu. Mambo haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado. 8 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na mitetemeko sehemu mbalimbali na njaa. Haya yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.
9 “Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kupigwa mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao. 10 Nayo habari njema lazima ihubiriwe kwanza kwa mataifa yote kabla ule mwisho haujawadia. 11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu.
12 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. 13 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
Chukizo La Uharibifu
(Mathayo 24:15-28; Luka 21:20-24)
14 “Mtakapoona ‘chukizo la uharibifu’ limesimama mahali pasipolipasa (asomaye na afahamu), basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani. 15Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke au kuingia ndani ili kuchukua chochote. 16Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. 17 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! 18Ombeni mambo haya yasitokee wakati wa baridi. 19 Kwa maana siku hizo zitakuwa za dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo, hapo Mungu alipoumba ulimwengu, mpaka leo, na wala haitakuwako tena kamwe. 20Kama Bwana asingelifupisha siku hizo, kamwe asingeliokoka mtu yeyote. Lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupisha siku hizo. 21 Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo#13:21 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. huyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msisadiki. 22 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule. 23 Hivyo jihadharini. Nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia.
Kuja Kwa Mwana Wa Adamu
(Mathayo 24:29-31; Luka 21:25-28)
24 “Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki,
“ ‘jua litatiwa giza
nao mwezi hautatoa nuru yake;
25 nazo nyota zitaanguka kutoka angani,
na nguvu za anga zitatikisika.’
26 “Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. 27 Naye atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.
Somo Kuhusu Mtini
(Mathayo 24:32-35; Luka 21:29-33)
28 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 29Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni. 30 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Hakuna Ajuaye Siku Wala Saa
(Mathayo 24:36-44)
32 “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. 33Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia. 34 Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe.
35 “Basi kesheni kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko. 36Kama akija ghafula, asije akawakuta mmelala. 37 Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’ ”