YouVersion Logo
Search Icon

Mithali 14

14
1 Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake,
bali mpumbavu huibomoa nyumba yake
kwa mikono yake mwenyewe.
2 Yeye ambaye njia zake ni nyofu humcha Bwana,
bali yeye ambaye njia zake zimepotoka humdharau Mungu.
3 Mazungumzo ya mpumbavu huleta fimbo mgongoni mwake,
bali mwenye hekima hulindwa na maneno ya midomo yake.
4 Pale ambapo hakuna mafahali, hori ni tupu,
bali kutokana na nguvu za fahali huja mavuno mengi.
5 Shahidi mwaminifu hadanganyi,
bali shahidi wa uongo humimina uongo.
6 Mwenye mzaha huitafuta hekima na haipati,
bali maarifa huja kwa urahisi kwa anayepambanua.
7Kaa mbali na mtu mpumbavu,
kwa maana hutapata maarifa katika midomo yake.
8 Hekima ya mwenye busara ni kufikiria njia zake,
bali upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.
9 Wapumbavu hudhihaki kujirekebisha kutoka dhambi,
bali wema hupatikana miongoni mwa wanyofu.
10Kila moyo hujua uchungu wake wenyewe,
wala hakuna yeyote awezaye kushiriki furaha yake.
11 Nyumba ya mwovu itaangamizwa,
bali hema la mnyofu litastawi.
12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu,
bali mwisho wake huelekeza mautini.
13 Hata katika kicheko moyo waweza kuuma,
nayo furaha yaweza kuishia katika majonzi.
14 Wasio na imani watapatilizwa kikamilifu kwa ajili ya njia zao,
naye mtu mwema atapewa thawabu kwa ajili ya njia yake.
15 Mtu mjinga huamini kila kitu,
bali mwenye busara hufikiria hatua zake.
16 Mtu mwenye hekima humcha Bwana na kuepuka mabaya,
bali mpumbavu hukasirika kwa hamaki na uzembe.
17 Mtu anayekasirika kwa haraka hufanya mambo ya upumbavu,
naye mtu wa hila huchukiwa.
18Mjinga hurithi upumbavu,
bali wenye busara huvikwa maarifa kichwani kama taji.
19 Watu wabaya watasujudu mbele ya watu wema,
nao waovu kwenye malango ya wenye haki.
20 Maskini huepukwa hata na majirani zao,
bali matajiri wana marafiki wengi.
21 Yeye anayemdharau jirani yake hutenda dhambi,
bali amebarikiwa yeye aliye na huruma kwa mhitaji.
22 Je, wale wanaopanga ubaya hawapotoki?
Bali wale wanaopanga kilicho chema
hupata upendo na uaminifu.
23Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida,
bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.
24 Utajiri wa wenye hekima ni taji yao,
bali upumbavu wa wapumbavu huzaa upumbavu.
25 Shahidi wa kweli huokoa maisha,
bali shahidi wa uongo ni mdanganyifu.
26 Yeye amchaye Bwana ana ngome salama,
na kwa watoto wake itakuwa kimbilio.
27 Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima,
ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.
28 Wingi wa watu ni utukufu wa mfalme,
bali pasipo watu mkuu huangamia.
29 Mtu mwenye subira ana ufahamu mwingi,
bali anayekasirika haraka huonyesha upumbavu.
30 Moyo wenye amani huupa mwili uzima,
bali wivu huozesha mifupa.
31 Yeye amwoneaye maskini huonyesha dharau kwa Muumba wao,
bali yeyote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu.
32 Waovu huangamizwa kwa matendo yao maovu,
bali hata katika kifo wenye haki hupata kimbilio.
33 Hekima hukaa katika moyo wa mwenye ufahamu
bali haijulikani miongoni mwa wapumbavu.
34 Haki huinua taifa,
bali dhambi ni aibu kwa watu wote.
35 Mfalme hupendezwa na mtumishi mwenye hekima,
bali ghadhabu yake humwangukia
mtumishi mwenye kuaibisha.

Currently Selected:

Mithali 14: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in