YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 28

28
Zaburi 28
Kuomba msaada
Zaburi ya Daudi.
1Ninakuita wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mwamba wangu;
usikatae kunisikiliza.
Kwa sababu ukinyamaza
nitafanana na walioshuka shimoni.
2Sikia kilio changu nikikuomba unihurumie,
ninapokuita ili unisaidie,
ninapoinua mikono yangu kuelekea
Patakatifu pa Patakatifu pako.
3Usiniburute pamoja na waovu,
pamoja na hao watendao mabaya,
ambao huzungumza na majirani zao maneno mazuri,
lakini mioyoni mwao wameficha chuki.
4Walipe sawasawa na matendo yao,
sawasawa na matendo yao maovu;
walipe sawasawa na kazi za mikono yao,
uwalipe wanavyostahili.
5Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Mwenyezi Mungu,
na yale ambayo mikono yake imetenda,
atawabomoa na kamwe
hatawajenga tena.
6Ahimidiwe Mwenyezi Mungu,
kwa maana amesikia kilio changu
nikimwomba anihurumie.
7Mwenyezi Mungu ni nguvu zangu na ngao yangu,
moyo wangu umemtumaini yeye,
nami nimesaidiwa.
Moyo wangu unarukaruka kwa furaha
nami nitamshukuru kwa wimbo.
8Mwenyezi Mungu ni nguvu ya watu wake,
ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.
9Waokoe watu wako na uubariki urithi wako;
uwe mchungaji wao na uwabebe milele.

Currently Selected:

Zaburi 28: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in