YouVersion Logo
Search Icon

1 Kor UTANGULIZI

UTANGULIZI
Waraka huu ni mmojawapo wa nyaraka za Paulo alizoziandikia Makanisa aliyoyaanzisha akiwa katika safari yake ya pili ya kitume. Paulo alikaa Korintho kwa muda wa miezi kumi na minane (Mdo 18:1-11). Korintho ulikuwa mji wa pwani wenye bandari iliyowavutia wasafiri na wafanya biashara. Bali na wenyeji walikuwamo Wagiriki, Warumi, Wasiria, Waasia, Wamisri na Wayahudi katika Korintho. Mji huu ulikuwa na sifa za maendeleo, anasa, na dini mbalimbali. “Kuishi kikorintho” ilimaanisha “uhuni” na “kupotea”.
Baada ya miaka michache Paulo, akiwa katika safari yake ya tatu ya kitume, alikaa Efeso kwa muda wa miaka mitatu (Mdo 19:1-41; 20:31). Akiwa huko aliarifiwa juu ya hali ya Korintho kwamba baadhi ya Wakristo walikuwa na matatizo yaliyohusu maisha adili. Paulo aliandika barua inayofikiriwa kuwa ya kwanza ili kutoa mawaidha yake juu ya hali hiyo (5:9). Barua hii haikuhifadhiwa. Vile vile aliwatuma Timotheo na Erasto wapitie Makedonia (Mdo 19–22), waende Korintho kuweka sawa Kanisa hilo (4:17; 16:10). Hata hivyo, baadaye kidogo, ujumbe ulitoka Korintho kuhusu hali mbaya iliyokuwa huko (1:11). Halafu kwa muda mfupi ukaja tena ujumbe mwingine ukiwa na masuala kadhaa kuhusu barua ya Paulo na kutaka maoni yake kuhusu matatizo yao (7:1; 16:17).
Paulo aliandika Waraka huu ili kushughulikia masuala ambayo waumini wa Korintho walitaka maelezo yake. Paulo aliyakabili mafarakano yaliyojitokeza wakati waumini walipokutana kumega mkate, zinaa miongoni mwa waumini, mashtaka kati ya Wakristo, matumizi mabaya ya uhuru wa kikristo, fujo katika kuadhimisha chakula cha Bwana, ukapera, ndoa, mjane, ibada kwa watu waliokufa, chakula kilichotambikiwa sanamu, suala la akina mama katika mikutano ya waumini, karama za Roho, na suala la ufufuo wa wafu. Katika mambo haya yote Paulo anatoa mwongozo wake jinsi ya kuishi kama mfuasi wa Kristo. Katika Waraka huu Paulo ametuachia baadhi ya mafundisho makuu ya nyaraka zake ikiwa ni pamoja na utenzi juu ya upendo (sura 13) na mafundisho juu ya msalaba wa Yesu (sura 1) na juu ya ufufuo (sura 15).

Currently Selected:

1 Kor UTANGULIZI: SUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in