7
Mfano kutoka kwa Sheria ya Ndoa
1Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? 2Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume. 3Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine. 4#Kol 2:14Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda. 5#Rum 6:21Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao. 6#Rum 8:1,2; 6:2,4Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.
Sheria na Dhambi
7 #
Kut 20:14,17; Kum 5:18,21 Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani. 8#Rum 5:13Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa. 9Nami nalikuwa hai hapo kwanza bila sheria; ila ilipokuja ile amri, dhambi ilihuika, nami nikafa. 10#Yak 1:15; Law 18:5Nikaona ile amri iletayo uzima ya kuwa kwangu mimi ilileta mauti. 11#Mwa 3:13Kwa maana dhambi, kwa kupata nafasi kwa ile amri, ilinidanganya, na kwa hiyo ikaniua. 12#1 Tim 1:8Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema. 13#Rum 5:20Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? Hasha! Bali dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa, ilifanya mauti ndani yangu kwa njia ya ile njema, kusudi kwa ile amri dhambi izidi kuwa mbaya mno.
Mzozo wa Kindani
14 #
Zab 51:5; Yn 3:6 Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. 15#Gal 5:17Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. 16Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. 17Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu 18#Mwa 6:5; 8:21Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. 19Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. 20Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. 21Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. 22Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, 23#Gal 5:17; Yak 4:1; 1 Pet 2:11lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. 24Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? 25#1 Kor 15:57Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.