YouVersion Logo
Search Icon

1 Yohana UTANGULIZI

UTANGULIZI
Nyaraka tatu ambazo huitwa za Yohana hazitaji jina la mwandishi wake. Mapokeo kutoka karne za kwanza Baada ya Kristo Kuzaliwa husema kuwa ni Yohana mwandishi wa Injili ya Yohana na Kitabu cha Ufunuo (tazama Utangulizi kwa Injili ya Yohana). Aliziandika Nyaraka hizo alipokuwa mzee akiwa anaishi kule Efeso. Aliyaandikia makanisa yaliyokuwa katika eneo hilo. Wataalamu wa mambo ya Biblia huziita “Nyaraka za Mzee”; wengine huziita, “Nyaraka za Kichungaji”.
Katika Waraka wa Kwanza, mwandishi anazungumzia “kufanyika mwili kwa Mwana wa Mungu”, “Uungu na Utu wa Yesu”, pamoja na sifa za Mungu yaani, nuru, uzima na upendo. Maisha safi na adili, yatawaliwayo na upendo, ni alama pekee ya ukristo.
Mwandishi wa Waraka huu anapinga mafundisho ya uongo yaliyotokana na watu waliojitakia kuwa na “ujuzi” fulani. Watu waliojitakia elimu au ujuzi huo (pengine wanatajwa kama “wapinga Kristo” – 2:18) walikataa kumtambua Yesu kama Kristo (2:22; 4:2) na hawatii amri ya upendo wa kindugu (2:9; 3:14).
Kwa hiyo mwandishi anawataka waumini waishi katika nuru, kwani Mungu ni nuru, na kuzingatia ile amri ya upendo (1:5—2:17). Wapinzani wa Kristo wapo, nao watakataa kwamba Yesu ndiye Kristo (2:18-29). Katika sura 3:1-24 watu walio kweli watoto wa Mungu wanabainishwa: maisha yaliyo sawa; upendo kati ya ndugu na uaminifu kwa Yesu Kristo. Katika 4:1-21 upendo asili yake ni Mungu na wanaomjua Mungu sharti wawe na upendo. Na mwishowe katika 5:1-21 mwandishi anazungumzia juu ya ushindi wa imani.

Currently Selected:

1 Yohana UTANGULIZI: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in