YouVersion Logo
Search Icon

2 Wakorintho UTANGULIZI

UTANGULIZI
Wakorintho walipopokea Waraka wa Kwanza wa Paulo na ujumbe wa Timotheo baadhi hawakuridhishwa na mwongozo wake na ziara ya Timotheo. Ule mpango wa kuwatembelea uliotangazwa katika 1 Kor 16:5-7 haukufanyika na waumini wa kule Korintho wakafikiri Paulo amekuwa kigeugeu kuhusu mipango yake (2 Kor 1:15-23). Paulo alikuwa amewatembelea kwa ajili ya kushughulikia hali hiyo (2:1), lakini ziara yake haikutatua matatizo, akarudi Efeso. Baadaye alipata taarifa kuwa waasi wanaendeleza uhasama. Paulo aliandika barua kali na yenye huzuni akaituma Korintho kwa mkono wa Tito. Ijapokuwa barua hii inatajwa katika Waraka huu (2:3-4,9; 7:8; 12:18) hatunayo katika Agano Jipya. Tito aliporudi alimkuta Paulo Makedonia (2:12-13; Mdo 20:1) akampasha habari nzuri yenye faraja kuwa Wakorintho wamebadili nia yao mbaya, wanatii mawaidha ya Paulo (7:5-6) na kuwaadhibu wafitini (2:5-11).
Paulo aliandika Waraka huu akautuma tena kwa mkono wa Tito na ndugu wengine wawili kule Korintho (8:16-18). Katika waraka huu Paulo anaeleza furaha yake juu ya kutubu kwao. Anaweka sawa yaliyokuwa yamepotoshwa katika kanisa. Katika sura 8-9, Paulo anasema kwa kirefu juu ya mchango kwa ajili ya kanisa la Yerusalemu (8:1—9:15). Katika sura 10—13, Paulo anatetea na kuthibitisha mamlaka yake kama Mtume na mtumishi wa Kristo.

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in