YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 13

13
Ufunuo juu ya Babeli
1 # Isa 47:1-15; Yer 50:1—51:64 Ufunuo juu ya Babeli; maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi.
2 # Yer 50:2; 51:25 Haya! Juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu. 3#Yoe 3:11 Mimi mwenyewe nimewaamuru watu wangu waliowekwa wakfu kwangu, naam, nimewaita watu wangu walio hodari kwa ajili ya hasira yangu, watu wangu wenye kiburi. 4Kelele milimani kama kelele za watu wengi sana; kelele za falme za mataifa waliokutana pamoja; BWANA wa majeshi anapanga jeshi kwa vita; 5watu waliotoka katika nchi iliyo mbali, tokea upande wa mwisho wa mbingu; naam, BWANA na silaha za ghadhabu yake, ili aiangamize nchi yote. 6#Amo 5:18; Sef 1:7; Ufu 6:17; Yoe 1:15 Pigeni kelele za hofu; maana siku ya BWANA i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. 7Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka. 8Nao watafadhaika; watashikwa na uchungu na maumivu; watakuwa na uchungu kama mwanamke aliye karibu kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto. 9#Mal 4:1 Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake. 10#Eze 32:7; Mt 24:29; Mk 13:24-25; Lk 21:15; Ufu 6:12-13 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze. 11Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayashusha chini majivuno yao walio wakali; 12nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri. 13#Yoe 3:16; Hag 2:6; Mt 24:29; Omb 1:12 Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya BWANA wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali. 14Basi, itakuwa kama vile paa aliyetishwa, na kama kondoo wasio na mtu wa kuwakusanya; kila mtu atageukia watu wake; nao watakimbia, kila mtu aende nchi yake mwenyewe. 15Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga. 16#Nah 3:10 Na watoto wao wachanga watavunjwavunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watanajisiwa. 17#Yer 51:11 Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu. 18Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto. 19#Mwa 19:24 Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. 20#Isa 14:23 Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko. 21#Isa 34:14; Sef 2:14; Ufu 18:2 Lakini huko watalala wanyama wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko. 22Na mbwamwitu watalia ndani ya ngome zake; na mbweha ndani ya majumba ya anasa; na wakati wake u karibu kufika, na siku zake hazitaongezeka.

Currently Selected:

Isaya 13: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in