YouVersion Logo
Search Icon

Matendo 4

4
Mitume Mbele ya Baraza Kuu la Wayahudi
1Petro na Yohana walipokuwa wanazungumza na watu, ghafla baadhi ya viongozi wa Kiyahudi waliwaendea. Walikuwepo baadhi ya makuhani, mkuu wa askari wanaolinda Hekalu na baadhi ya Masadukayo. 2Walikasirika kwa sababu ya mafundisho ambayo Petro na Yohana walikuwa wanawafundisha na kuwaambia watu kuhusu Yesu. Mitume walikuwa wanafundisha pia kwamba watu watafufuka kutoka kwa wafu. 3Waliwakamata Petro na Yohana. Kwa kuwa ilikuwa jioni tayari, waliwaweka gerezani usiku ule mpaka siku iliyofuata. 4Lakini watu wengi waliowasikia mitume waliamini walichosema. Na siku hiyo idadi ya watu katika kundi la waamini ikafikia watu 5,000.
5Siku iliyofuata, watawala wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria walikutana Yerusalemu. 6Kuhani mkuu Anasi alikuwepo. Kayafa, Yohana, Iskanda na jamaa wengine wa kuhani mkuu walikuwepo pia. 7Waliwasimamisha Petro na Yohana mbele ya watu wote. Wakawauliza maswali mengi, “Mliwezaje kumponya mlemavu wa miguu huyu? Mlitumia nguvu gani? Mmefanya hili kwa mamlaka ya nani?”
8Ndipo Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akawaambia, “Enyi watawala nanyi wazee wa watu, 9mnatuuliza leo ni nini tulifanya kumsaidia huyu mlemavu wa miguu? Mnatuuliza nini kilimponya? 10Tunataka ninyi nyote na watu wote wa Israeli mtambue kuwa mtu huyu aliponywa na nguvu ya Yesu Kristo kutoka Nazareti. Mlimpigilia Yesu msalabani, lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Mtu huyu alikuwa mlemavu wa miguu, lakini sasa ni mzima. Anaweza kusimama hapa mbele zenu kwa sababu ya nguvu ya Yesu! 11Yesu ndiye
‘Jiwe#4:11 Jiwe Alama kumaanisha Yesu. ambalo ninyi wajenzi mlilikataa.
Lakini jiwe hili limekuwa jiwe na msingi.’#Zab 118:22
12Yesu peke yake ndiye anayeweza kuokoa watu. Jina lake ndiyo nguvu pekee iliyotolewa kumwokoa mtu yeyote ulimwenguni. Ni lazima tuokoke kupitia yeye!”
13Viongozi wa Kiyahudi walijua kuwa Petro na Yohana walikuwa watu wa kawaida wasio na elimu yoyote. Lakini walikuwa wanazungumza kwa ujasiri bila woga; viongozi walishangaa. Walitambua pia kuwa Petro na Yohana walikuwa pamoja na Yesu. 14Walimwona aliyeponywa akiwa amesimama kwa miguu yake mwenyewe pembeni mwa mitume. Na hivyo walishindwa kuzungumza chochote kilicho kinyume na mitume.
15Viongozi wa Kiyahudi wakawaambia mitume watoke nje ya chumba cha mkutano wa baraza. Kisha viongozi wakajadiliana wao wenyewe juu ya nini wanachopaswa kufanya. 16Wakaulizana, “Tuwafanye nini watu hawa? Kila mtu katika Yerusalemu anajua kuhusu muujiza walioufanya kama ishara kutoka kwa Mungu. Ni dhahiri, hatuwezi kusema muujiza huo haukufanyika. 17Lakini ni lazima tuwatishe ili wasiendelee kuwaambia watu kutumia jina lile.#4:17 jina lile Yaani, jina la Yesu. Viongozi wa Kiyahudi walikwepa kutamka jina lake. Tazama Lk 15:2 na Mdo 5:28. Ili tatizo hili lisisambae miongoni mwa watu.”
18Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaita Petro na Yohana ndani tena. Wakawaambia wasiseme wala kufundisha kitu chochote kwa kutumia jina la Yesu. 19Lakini Petro na Yohana wakawajibu, “Mnadhani kipi ni sahihi? Mungu angetaka nini? Je! tunapaswa kuwatii ninyi au tumtii Mungu? 20Hatuwezi kukaa kimya. Ni lazima tuwaambie watu kuhusu yale tuliyoona na kusikia.”
21-22Viongozi wa Kiyahudi hawakupata sababu za kuwaadhibu mitume, kwa sababu watu wote walikuwa wanamsifu Mungu kwa kile kilichotendeka. Muujiza huu ulikuwa ishara kutoka kwa Mungu. Mtu aliyeponywa alikuwa na miaka zaidi ya arobaini. Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaonya mitume tena na kuwaacha waende wakiwa huru.
Petro na Yohana Warudi kwa Waamini
23Petro na Yohana waliondoka kwenye mkutano wa viongozi wa Kiyahudi na kurudi kwa waamini wenzao. Wakalieleza kundi la waamini kila kitu walichoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 24Waamini waliposikia hili, wote kwa pamoja wakamwomba Mungu wakiwa na nia moja. Wakasema, “Bwana wa wote, wewe ndiye uliyeumba mbingu, dunia, bahari na kila kitu ulimwenguni. 25Baba yetu Daudi alikuwa mtumishi wako. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliandika maneno haya:
‘Kwa nini mataifa yanatenda kwa kiburi?
Kwa nini watu wanapanga mipango isiyofaa kama hii?
26Wafalme wa dunia hujiandaa kwa mapigano,
na watawala hukusanyika pamoja kinyume na Bwana
na kinyume na Masihi wake.’#Zab 2:1-2
27Ndicho hasa kilichotokea wakati Herode, Pontio Pilato, mataifa mengine na watu wa Israeli walipokusanyika pamoja hapa Yerusalemu wakawa kinyume na Yesu; Masihi, Mtumishi wako mtakatifu. 28Watu hawa waliokusanyika pamoja kinyume na Yesu waliwezesha mpango wako kukamilika. Ilifanyika kwa sababu ya nguvu zako na matakwa yako. 29Na sasa, Bwana, sikiliza wanayosema. Wanajaribu kututisha. Sisi ni watumishi wako. Tusaidie ili tuseme yale unayotaka tuseme bila kuogopa. 30Tusaidie, ili tuwe jasiri kwa kutuonesha nguvu zako. Ponya Wagonjwa. Fanya ishara na maajabu kutokea kwa mamlaka#4:30 mamlaka Kwa maana ya kawaida, “Katika jina la Yesu”. ya Yesu mtumishi wako mtakatifu.”
31Baada ya waamini kuomba, mahali walipokuwa palitikisika. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, na wakaendelea kuhubiri Habari Njema bila woga.
Ushirika wa Waamini
32Kundi lote la waamini waliungana katika kuwaza na katika mahitaji yao. Hakuna aliyesema vitu alivyokuwa navyo ni vyake peke yake. Badala yake walishirikiana kila kitu. 33Kwa nguvu kuu mitume walifanya ijulikane kwa kila mmoja kwamba Bwana Yesu alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na Mungu aliwabariki sana waamini wote. 34Hakuna aliyepungukiwa kitu. Kila aliyemiliki shamba au nyumba aliuza na kuleta pesa alizopata, 35na kuzikabidhi kwa mitume. Kisha kila mtu akapewa kiasi alichohitaji.
36Mmoja wa waamini aliitwa Yusufu. Mitume walimwita Barnaba, jina linalomaanisha “Mtu anayewatia moyo wengine.” Alikuwa Mlawi mzaliwa wa Kipro. 37Yusufu aliuza shamba alilomiliki. Akaleta pesa na kuwapa mitume.

Currently Selected:

Matendo 4: TKU

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in