YouVersion Logo
Search Icon

Luka 18

18
Mungu Atawajibu Watu Wake
1Kisha Yesu akawafundisha wafuasi wake kwamba wanapaswa kuomba daima bila kupoteza tumaini. Akatumia simulizi hii kuwafundisha. 2Akasema, “Kulikuwa na mwamuzi katika mji fulani. Hakumcha Mungu wala hakujali watu walikuwa wanamfikiriaje. 3Na katika mji huo huo alikuwepo mwanamke mjane. Huyu alimjia mwamuzi huyu mara nyingi akimwambia, ‘Kuna mtu anayenitendea mambo mabaya. Nipe haki yangu!’ 4Mwanzoni mwamuzi hakutaka kumsaidia yule mwanamke. Lakini baada ya muda kupita, akawaza moyoni mwake yeye mwenyewe, ‘Simchi Mungu. Na sijali watu wananifikiriaje. 5Lakini mwanamke huyu ananisumbua. Nikimpa haki yake ataacha kunisumbua. Nisipomsaidia, ataendelea kunijia na anaweza kunishambulia.’”
6Bwana akasema, “Sikilizeni, maneno aliyosema mwamuzi mbaya yana mafundisho kwa ajili yenu. 7Daima Mungu atawapa mahitaji yao wateule wanaomwomba usiku na mchana. Hatachelewa kuwajibu. 8Ninawaambia, Mungu atawapa haki yao watu wake haraka. Lakini Mwana wa Adamu atakaporudi, atawakuta duniani watu ambao bado wanamwamini?”
Farisayo na Mtoza Ushuru
9Walikuwepo baadhi ya watu waliojiona kuwa wenye haki na waliwadharau wengine. Yesu alitumia simulizi hii kuwafundisha: 10“Siku moja Farisayo na mtoza ushuru walikwenda Hekaluni kuomba. 11Farisayo alisimama peke yake mbali na mtoza ushuru. Farisayo aliomba akisema, ‘Ee Mungu, ninakushukuru kwa kuwa mimi si mwovu kama watu wengine. Mimi siyo kama wezi, waongo au wazinzi. Ninakushukuru kwa kuwa mimi ni bora kuliko huyu mtoza ushuru. 12Ninafunga mara mbili kwa wiki na kutoa sehemu ya kumi ya vyote ninavyopata!’
13Mtoza ushuru alisimama peke yake pia. Lakini alipoanza kuomba, hakuthubutu hata kutazama juu mbinguni. Alijipigapiga kifua chake akijinyenyekeza mbele za Mungu. Akasema, ‘Ee Mungu, unihurumie, mimi ni mwenye dhambi.’ 14Ninawaambia, mtu huyu alipomaliza kuomba na kwenda nyumbani, alikuwa amepatana na Mungu. Lakini Farisayo, aliyejisikia kuwa bora kuliko wengine, hakuwa amepatana na Mungu. Watu wanaojikweza watashushwa. Lakini wale wanaojishusha watakwezwa.”
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mt 19:13-15; Mk 10:13-16)
15Baadhi ya watu waliwaleta hata watoto wao wadogo kwa Yesu ili awawekee mikono kuwabariki. Lakini wafuasi walipoona hili, waliwakataza. 16Lakini Yesu aliwaalika watoto kwake na kuwaambia wafuasi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto wadogo hawa. 17Ukweli ni kwamba, ni lazima uupokee ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyopokea vitu, la si hivyo hautauingia.”
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mt 19:16-30; Mk 10:17-31)
18Kiongozi wa dini akamuuliza Yesu, “Mwalimu Mwema, ni lazima nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?”
19Yesu akamwambia, “Kwa nini unaniita mwema? Mungu peke yake ndiye mwema. 20Na unazijua amri zake: ‘Usizini, usiue, usiibe, usiseme uongo, na ni lazima uwaheshimu baba na mama yako.’”#Kut 20:12-16; Kum 5:16-20
21Lakini yule kiongozi akasema, “Nimezitii amri zote hizi tangu nilipokuwa mdogo.”
22Yesu aliposikia hili, akamwambia, “Lakini kuna jambo moja unatakiwa kufanya. Uza kila kitu ulichonacho na uwape maskini pesa. Utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha, njoo unifuate.” 23Lakini yule mtu aliposikia Yesu anamwambia kutoa pesa zake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa sababu alikuwa tajiri sana.
24Yesu alipoona kuwa amehuzunika, akasema, “Itakuwa vigumu sana kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 25Ni rahisi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
26Watu waliposikia hili, wakasema, “Sasa ni nani anayeweza kuokolewa?”
27Yesu akajibu, “Lisilowezekana kwa wanadamu, linawezekana kwa Mungu.”
28Petro akasema, “Tazama! Tumeacha vyote tulivyokuwa navyo na kukufuata.”
29Yesu akasema, “Ninaahidi kuwa kila aliyeacha nyumba, mke, ndugu, wazazi, au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu, 30atapokea zaidi ya kile alichoacha. Atapokea mara nyingi zaidi katika maisha haya. Na katika ulimwengu ujao atapata mara nyingi zaidi.”
Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake
(Mt 20:17-19; Mk 10:32-34)
31Kisha Yesu alizungumza na mitume wake kumi na mbili wakiwa peke yao. Akawaaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu. Kila kitu ambacho Mungu aliwaambia manabii waandike kuhusu Mwana wa Adamu kitatokea. 32Atakabidhiwa kwa wasio Wayahudi, ambao watamcheka, watamtukana na kumtemea mate. 33Watamchapa kwa mijeledi kisha watamuua. Lakini katika siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuka kutoka kwa wafu.” 34Mitume walijaribu kulielewa hili, lakini hawakuweza; maana yake ilifichwa wasiielewe.
Yesu Amponya Asiyeona
(Mt 20:29-34; Mk 10:46-52)
35Yesu alipofika karibu na mji wa Yeriko, mwanaume mmoja asiyeona alikuwa amekaa kando ya barabara, akiomba pesa. 36Aliposikia kundi la watu linapita barabarani, akauliza, “Nini kimetokea?”
37Walimwambia, “Yesu kutoka Nazareti anapitia hapa.”
38Kipofu akapasa sauti yake, akaita, “Yesu, Mwana wa Daudi, tafadhali nisaidie!”
39Watu waliotangulia, wakiongoza kundi, wakamkanya asiyeona, wakamwambia anyamaze. Lakini alizidi sana kupaza sauti zaidi na zaidi, “Mwana wa Daudi, tafadhali unisaidie!”
40Yesu alisimama pale na akasema, “Mleteni yule asiyeona kwangu!” Yule asiyeona alipofika kwa Yesu, Yesu akamwuliza, 41“Unataka nikufanyie nini?”
Asiyeona akasema, “Bwana, nataka kuona.”
42Yesu akamwambia, “Unaweza kuona sasa. Umeponywa kwa sababu uliamini.”
43Yule mtu akaanza kuona saa ile ile. Akamfuata Yesu, akimshukuru Mungu. Kila mtu aliyeliona hili alimsifu Mungu.

Currently Selected:

Luka 18: TKU

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in