UTANGULIZI
Jina la kitabu hiki latokana na mtu mashuhuri ambaye anahusika sana katika mambo tunayosimuliwa humu, yaani Yoshua. Yoshua alipewa jukumu la kuwaongoza Waisraeli baada ya kifo cha Mose. Aliwaongoza Waisraeli mpaka walipoiteka ile nchi ambayo Mungu alikuwa ameahidi kuwapa. Kitabu hiki chaeleza jinsi Waisraeli walivyoingia nchini Kanaani, wakaimiliki nchi hiyo na kuigawa. Kadhalika kitabu chenyewe chaonesha wazi kwamba ahadi ile ambayo Mungu aliwapa wazee wa Israeli na Mose imekamilika, maana Waisraeli sasa wameweza kutua katika nchi hiyo na kukaa (tazama kwa mfano, 11:23; 21:43-45 na sura ya 23).
Kitabu hiki kina sehemu tatu:
Sura 1–12: Nchi ya upande wa magharibi ya mto Yordani inavamiwa. Kwanza kuna matayarisho ya kuivamia. Yoshua anahakikishiwa na Mungu kwamba, kwa msaada wake, watafaulu katika shughuli hiyo. Makabila mawili na nusu ambayo yalikwenda mashariki ya mto Yordani na kukaa huko, yalimuunga mkono Yoshua. Wapelelezi walipelekwa kupeleleza juu ya mji wa Yeriko, wakarudi na habari za kutia moyo. Kisha Waisraeli walivuka mto Yordani. Halafu tunaambiwa jinsi watu walivyouteka mji wa Yeriko. Hatimaye tunaelezwa juu ya kutekwa kwa mji wa Ai na baadaye juu ya agano kati ya Waisraeli na watu wa Gibeoni, na mwishowe tunaambiwa jinsi sehemu ya kusini ya Kanaani ilivyotekwa.
Sura 13–22: Kwanza tunaelezwa juu ya sehemu za nchi hiyo ambazo zilikuwa bado hazijachukuliwa na Waisraeli, kisha tunaambiwa jinsi nchi hiyo itakavyogawanyiwa makabila ya Israeli. Sehemu hii inamalizika kwa habari za kurejea kwa makabila ya mashariki katika sehemu yao wenyewe na kujengwa kwa madhabahu huko Yordani.
Sura 23–24: Zinaeleza shughuli za Yoshua na kutupa hotuba mbili za mwisho za kuwaaga Waisraeli. Yoshua anawahimiza Waisraeli waachane na miungu ya uongo, wachague kumtumikia Mwenyezi-Mungu peke yake. Mwishowe tunapewa habari za kifo cha Yoshua na kuhani Eleazari.