YouVersion Logo
Search Icon

Yobu 22

22
Hoja ya Elifazi
1Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu Yobu:
2“Je, binadamu anafaa chochote kwa Mungu?
Kwa kweli mwenye hekima anajifaidi mwenyewe tu.
3Je, unadhani wamfurahisha Mungu kwa kuwa mnyofu?
Au anapata faida gani kama huna hatia?
4Unadhani anakurudi na kukuhukumu
kwa sababu wewe unamheshimu?
5La! Uovu wako ni mkubwa mno!
Ubaya wako hauna mwisho!
6Wewe umemnyanganya ndugu yako nguo ya rehani;
umemchukulia nguo hiyo moja aliyokuwa nayo.
7Umewanyima maji wale waliokuwa wamechoka;
umewanyima chakula wale walio na njaa.
8Umemruhusu mwenye cheo kuchukua ardhi yote;
umemwacha anayependelewa aishi humo.
9Umewaacha wajane waende mikono mitupu;
umewanyima yatima uwezo wao.
10Kwa hiyo mitego imekuzunguka pande zote,
hofu ya ghafla imekuvamia.
11Giza limekuangukia usione kitu;
mafuriko ya maji yamekufunika.
12Twajua Mungu yuko huko juu mbinguni.
Tazama nyota za juu kabisa zilivyo mbali!
13Lakini wewe wasema: ‘Mungu ajua nini?
Je, aweza kupenya mawingu akatoa hukumu?
14Mawingu mazito yamemzunguka asipate kuona
yeye hutembea nje ya anga la dunia!’
15“Je, umeamua kufuata njia za zamani
ambazo watu waovu wamezifuata?
16Hao walifagiliwa kabla ya wakati wao,
misingi yao ilikumbwa mbali na maji.
17Hao ndio waliomwambia Mungu, ‘Achana nasi!’
Na ‘Wewe Mungu Mwenye Nguvu waweza nini juu yetu?’
18Lakini Mungu ndiye aliyejaza nyumba zao fanaka,
lakini walimweka mbali na mipango yao!#22:18 lakini … yao: Taz 21:16.
19Wanyofu huona na kufurahi,
wasio na hatia huwacheka na kuwadharau,
20Wanasema ama kweli maadui zetu wameangamizwa,
na walichobakiza kimeteketezwa kwa moto.
21“Sasa, Yobu, kubaliana na Mungu uwe na amani,
na hapo mema yatakujia.
22Pokea mafundisho kutoka kwake;
na yaweke maneno yake moyoni mwako.
23Ukimrudia Mungu na kunyenyekea,
ukiondoa uovu mbali na makao yako,
24ukitupilia mbali mali yako,
ukaitupa dhahabu ya Ofiri ukingoni mwa kijito,
25Mungu Mwenye Nguvu akawa ndio dhahabu yako,
na fedha yako ya thamani;
26basi, ndipo utakapomfurahia Mungu mwenye nguvu
na kutazama kwa matumaini;
27utamwomba naye atakusikiliza,
nawe utazitimiza nadhiri zako.
28Chochote utakachoamua kitafanikiwa,
na mwanga utaziangazia njia zako.
29Maana, Mungu huwaporomosha wenye majivuno,
lakini huwaokoa wanyenyekevu.
30Yeye humwokoa mtu asiye na hatia;
wewe utaokolewa kwa matendo yako mema.”

Currently Selected:

Yobu 22: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in