YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 39

39
Binadamu mbele ya Mungu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi)
1Nilisema: “Nitayachunga maisha yangu,
nisije nikatenda dhambi kwa usemi wangu.
Nitafunga mdomo wangu waovu wawapo karibu nami.”
2Nilikuwa kama bubu, bila kusema kitu,
nilinyamaza lakini sikupata nafuu.
Mateso yangu yalizidi kuwa makali,
3mahangaiko yangu yakaniunguza moyoni.
Kadiri nilivyowaza ndivyo nilivyotaabika,
kisha maneno haya yakanitoka:
4“Ee Mwenyezi-Mungu, unijulishe mwisho wangu,
siku zangu za kuishi zimenibakia ngapi,
nijue yapitavyo kasi maisha yangu!”
5Kumbe umenipimia maisha mafupi sana!
Maisha yangu si kitu mbele yako.
Hakika, kila binadamu ni kama pumzi tu!
6Kweli, kila mtu anapita kama kivuli;
jitihada zake zote ni bure tu;
anakusanya mali, asijue atakayeipata!
7Na sasa, ee Bwana, ninatazamia nini?
Tumaini langu ni kwako wewe!
8Uniokoe katika makosa yangu yote;
usikubali wapumbavu wanidhihaki.
9Niko kama bubu, sisemi kitu,
kwani wewe ndiwe uliyetenda hayo.
10Usiniadhibu tena;
namalizika kwa mapigo yako.
11Unapomwadhibu mtu dhambi zake kwa kumkemea,
unaharibu kama nondo kile akipendacho.
Hakika, kila binadamu ni kama pumzi tu!
12Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu;
usikilize kilio changu,
usikae kimya ninapolia.
Maana, mimi ni kama mgeni tu apitaye,
ni msafiri kama walivyokuwa wazee wangu wote.
13Uache kunitazama nipate kufurahi kidogo,
kabla sijaaga dunia, na kutoweka kabisa.

Currently Selected:

Zaburi 39: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in