Yohana 6

6
Kuwalisha watu elfu tano
1 # Mt 14:13-21; 15:32-39; Mk 6:32-44; 8:1-10; Lk 9:10-17 Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. 2Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. 3Naye Yesu akapanda mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. 4#Yn 2:13; 11:55; Lk 22:1 Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. 5Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? 6Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. 7Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. 8Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, 9#2 Fal 4:42,43 Yupo hapa mtoto, ana mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? 10Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi wanaume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. 11Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. 12Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee chochote. 13Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. 14#Kum 18:15 Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni.
15 # Yn 18:36 Kisha Yesu, alipotambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.
Yesu atembea juu ya maji
16 # Mt 14:22-33; Mk 6:45-52 Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakateremka baharini 17wakapanda katika mashua, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. 18Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. 19Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kuikaribia mashua; wakaogopa. 20Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. 21Basi wakataka kumpokea katika mashua; na mara hiyo mashua ikaifikia nchi waliyokuwa wakiiendea.
22Kesho yake mkutano waliosimama ng'ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja, tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao, 23#Yn 6:11 (lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru.) 24Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. 25Hata walipomwona ng'ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?
26Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27#Yn 4:14; 5:36; Mt 16:12 Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa mhuri na Baba, yaani, Mungu. 28Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? 29#1 Yoh 3:23 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye. 30#Yn 2:18; Mk 8:11 Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? 31#Kut 16:4,15; Zab 78:24 Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. 32#Yn 6:49 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Sio Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. 33#Yn 6:51 Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. 34Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. 35#Yn 4:14; 6:48; 7:37 Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. 36#Yn 6:26,29 Lakini niliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. 37#Yn 17:6-8; Mt 11:28 Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. 38#Yn 4:34; Mt 26:39 Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenituma. 39#Yn 10:28,29; 17:12 Na mapenzi yake aliyenituma ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. 40#Yn 5:29; 11:24 Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
41Basi Wayahudi wakamnung'unikia, kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. 42#Lk 4:22 Wakasema, Je! Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni? 43Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung'unike ninyi kwa ninyi. 44#Yn 6:55 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenituma; nami nitamfufua siku ya mwisho. 45#Isa 54:13; Yer 31:33,34 Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. 46#Yn 1:18 Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. 47#Yn 3:16 Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye anao uzima wa milele. 48#Yn 6:35 Mimi ndimi chakula cha uzima. 49#Yn 6:31,32; 1 Kor 10:3,5 Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. 50Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. 51#Ebr 10:5,10 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.
52 # Yn 6:60 Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? 53Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. 55Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56#Yn 15:4; 1 Yoh 3:24; 2:24 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. 57Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. 58Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. 59Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu.
Maneno ya uzima wa milele
60Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? 61Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung'unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza? 62#Yn 3:13 Itakuwaje basi, mumwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? 63#2 Kor 3:6 Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. 64#Yn 13:11 Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. 65#Yn 6:44 Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.
66Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. 67Basi Yesu akawaambia wale Kumi na Wawili, Je! Ninyi nanyi mnataka kuondoka? 68#Mt 16:16; Mk 8:29; Lk 9:20; Yn 6:63 Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 69#Yn 1:49; 11:27; Mt 14:33; 16:16 Nasi tumeamini, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu. 70Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Kumi na Wawili, na mmoja wenu ni shetani? 71Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Kumi na Wawili.

S'ha seleccionat:

Yohana 6: SRUVDC

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió