Mathayo 10

10
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mk 3:13-19; 6:7-13; Lk 6:12-16; 9:1-6)
1Yesu aliwaita pamoja wafuasi wake kumi na mbili. Akawapa uwezo juu ya pepo wabaya ili waweze kuwafukuza na pia kuponya kila aina ya magonjwa na maradhi. 2Haya ni majina ya mitume kumi na wawili:
Simoni (ambaye pia aliitwa Petro),
Andrea, kaka yake Petro,
Yakobo, mwana wa Zebedayo,
Yohana, kaka yake Yakobo,
3Filipo,
Bartholomayo,
Thomaso,
Mathayo, mtoza ushuru,
Yakobo, mwana wa Alfayo,
Thadayo,
4Simoni Mzelote,
Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu).
5Yesu aliwatuma mitume hawa kumi na wawili pamoja na maelekezo haya: “Msiende kwa watu wasio Wayahudi. Na msiingie katika miji ambako Wasamaria wanaishi. 6Lakini nendeni kwa watu wa Israeli. Wako kama kondoo waliopotea. 7Mtakapokwenda, waambieni hivi: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’ 8Waponyeni wagonjwa. Fufueni waliokufa. Waponyeni watu wenye magonjwa mabaya sana ya ngozi. Na toeni mashetani kwa watu. Ninawapa nguvu hii bure, hivyo wasaidieni wengine bure. 9Msibebe pesa pamoja nanyi; dhahabu au fedha au shaba nyekundu. 10Msibebe mikoba. Chukueni nguo na viatu mlivyovaa tu. Na msichukue fimbo ya kutembelea. Mfanyakazi anastahili kupewa anachohitaji.
11Mnapoingia katika mji, tafuteni kwa makini hadi mumpate mtu anayefaa na mkae katika nyumba yake mpaka mtakapoondoka mjini. 12Mtakapoingia katika nyumba hiyo, semeni, ‘Amani iwe kwenu.’ 13Ikiwa watu katika nyumba hiyo watawakaribisha, wanastahili amani yenu. Wapate amani mliyowatakia. Lakini ikiwa hawatawakaribisha, hawastahili amani yenu. Ichukueni amani mliyowatakia. 14Na ikiwa watu katika nyumba au mji watakataa kuwapokea au kuwasikiliza, basi ondokeni mahali hapo na mkung'ute mavumbi kutoka katika miguu yenu. 15Ninaweza kuwathibitishia kuwa siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa mji huo kuliko watu wa Sodoma na Gomora.#10:15 Sodoma na Gomora Miji ambayo Mungu aliiangamiza kwa sababu watu waliokuwa wakiishi pale walikuwa waovu sana. Tazama Mwa 19.
Yesu Aonya Kuhusu Matatizo
(Mk 13:9-13; Lk 21:12-17)
16Sikilizeni! Ninawatuma, nanyi mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Hivyo muwe na akili kama nyoka. Lakini pia muwe kama njiwa na msimdhuru yeyote. 17Muwe waangalifu! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka ili kuwashitaki mbele ya mabaraza ya mijini. Watawachapa ndani ya masinagogi yao. 18Mtasimamishwa mbele ya magavana na wafalme. Watu watawafanyia ninyi hivi kwa sababu mnanifuata. Mtakuwa mashahidi wangu mbele za wafalme na magavana hao na kwa watu wa mataifa mengine. 19Mtakapokamatwa, msisumbuke kuhusu nini mtakachosema au namna gani mtakavyosema. Katika wakati huo mtapewa maneno ya kusema. 20Si ninyi mtakaoongea; Roho wa Baba Mungu wenu atakuwa anaongea kupitia ninyi.
21Ndugu watakuwa kinyume cha ndugu zao wenyewe na kuwapeleka kwenda kuuawa. Baba watawapeleka watoto wao wenyewe kuuawa. Watoto watapigana kinyume na wazazi wao na watawapeleka kuuawa. 22Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. Lakini atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 23Mnapotendewa vibaya katika mji mmoja, nendeni katika mji mwingine. Ninawaahidi kuwa hamtamaliza kwenda katika miji ya Israeli kabla Mwana wa Adamu hajarudi.
24Wanafunzi si wazuri kuliko mwalimu wao. Watumwa si wazuri kuliko bwana wao. 25Inatosha kwa wanafunzi kuwa kama walimu wao na watumwa kuwa kama bwana wao. Iwapo watu hao wananiita ‘mtawala wa pepo’, na mimi ni kiongozi wa familia, basi ni dhahiri kwa kiasi gani watawatukana ninyi, mlio familia yangu!
Mwogopeni Mungu, Siyo Watu
(Lk 12:2-7)
26Hivyo msiwagope watu hao. Kila kitu kilichofichwa kitaoneshwa. Kila kilicho siri kitajulikana. 27Ninayowaambia ninyi faraghani myaseme hadharani. Kila ninachowanong'oneza nawataka mkiseme kwa sauti kila mtu asikie.
28Msiwaogope watu. Wanaweza kuua mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Mnapaswa kumwogopa Mungu, anayeweza kuuharibu mwili na roho jehanamu. 29Ndege wanapouzwa, ndege wawili wadogo hugharimu senti moja tu. Lakini hakuna hata mmoja wa ndege hao wadogo anaweza kufa bila Baba yenu kufahamu. 30Mungu anafahamu idadi ya nywele katika vichwa vyenu. 31Hivyo msiogope. Mna thamani kuliko kundi kubwa la ndege.
Msiionee Haya Imani Yenu
(Lk 12:8-9)
32Iwapo mtawaambia watu wengine kuwa mnaniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi ni wangu. 33Lakini ikiwa mtasimama mbele ya wengine na kusema kuwa hamniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi si wangu.
Kumfuata Yesu Kunaleta Matatizo
(Lk 12:51-53; 14:26-27)
34Msidhani kuwa nilikuja duniani kuleta amani. Sikuja kuleta amani. Nilikuja kuleta vita. 35Nimekuja ili hili litokee:
‘Mwana atamgeuka baba yake.
Binti atamgeuka mama yake.
Binti mkwe atamgeuka mama mkwe wake.
36Hata watu wa familia zenu watakuwa adui zenu.’#10:35-36 Tazama Mik 7:6
37Wale wanaowapenda baba zao au mama zao kuliko wanavyonipenda mimi hawana thamani kwangu. Na wale wanaowapenda wana wao au binti zao kuliko wanavyonipenda mimi hawastahili kuwa wafuasi wangu. 38Wale ambao hawataupokea msalaba waliopewa wanaponifuata hawastahili kuwa wanafunzi wangu na kunifuata. 39Wale wanaojaribu kuyatunza maisha waliyonayo, watayapoteza. Lakini wale wanaoyaacha maisha yao kwa ajili yangu watapata uzima halisi.
Mungu Atawabariki Wanaowakaribisha Ninyi
(Mk 9:41)
40Yeyote anayewakubali ninyi ananikubali mimi. Na yeyote anayenikubali anamkubali yule aliyenituma. 41Yeyote anayemkubali nabii kwa sababu ni nabii atapata ujira wa nabii. Na yeyote anayemkubali mwenye haki kwa sababu ni mwenye haki atapata ujira anaoupata mwenye haki. 42Yeyote anayemsaidia mmoja wa wafuasi wangu hawa wanyenyekevu kwa sababu ni wafuasi wangu hakika atapata ujira, hata ikiwa wanawapa tu kikombe cha maji baridi.”

S'ha seleccionat:

Mathayo 10: TKU

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió