Mathayo 26

26
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mk 14:1-2; Lk 22:1-2; Yh 11:45-53)
1Yesu alipomaliza akasema haya yote, akawaambia wafuasi wake, 2“Mnajua kuwa kesho kutwa ni Pasaka. Siku hiyo Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwa maadui zake ili auawe msalabani.”
3Ndipo viongozi wa makuhani na wazee walikutana katika nyumba ya Kayafa kuhani mkuu. 4Katika mkutano huo walitafuta njia ya kumkamata na kumwua Yesu kwa siri pasipo mtu yeyote kujua. 5Wakasema, “Hatuwezi kumkamata Yesu wakati wa sherehe ya Pasaka. Hatutaki watu wakasirike na kusababisha vurugu.”
Mwanamke Ampa Yesu Heshima
(Mk 14:3-9; Yh 12:1-8)
6Yesu alipokuwa Bethania katika nyumba ya Simoni aliyekuwa na ugonjwa hatari sana wa ngozi. 7Mwanamke alimwendea, akiwa na chupa yenye manukato ya thamani kubwa. Yesu akiwa anakula, mwanamke huyo akamwagia manukato hayo kichwani.
8Wanafunzi walipomwona mwanamke akifanya hivi walimkasirikia. Walisema, “Kwa nini kuharibu manukato hayo? 9Yangeuzwa na pesa nyingi ingepatikana, na pesa hiyo wangepewa maskini.”
10Lakini Yesu alijua kilichokuwa kinaendelea. Akasema, “Kwa nini mnamsumbua mwanamke huyu? Amenifanyia jambo zuri sana. 11Mtaendelea kuishi na maskini siku zote.#26:11 Mtaendelea kuishi na maskini siku zote Tazama Kum 15:11. Lakini ninyi hamtakuwa nami siku zote. 12Mwanamke huyu amenimwagia manukato. Amefanya hivi kuniandaa kwa ajili ya mazishi baada ya kufa. 13Habari Njema itahubiriwa kwa watu wote ulimwenguni. Na ninaweza kuwathibitishia kuwa kila mahali ambako Habari Njema zitahubiriwa, jambo alilofanya mwanamke huyu litahubiriwa pia, na watu watamkumbuka.”
Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu
(Mk 14:10-11; Lk 22:3-6)
14Ndipo Yuda Iskariote, mmoja wa wanafunzi kumi na wawili wa Yesu alikwenda kuzungumza na wakuu wa makuhani. 15Akasema, “Nikimkabidhi Yesu kwenu, mtanilipa nini?” Makuhani walimpa sarafu thelathini za fedha. 16Kuanzia siku hiyo, Yuda alianza kutafuta muda mzuri wa kumsaliti Yesu.
Karamu ya Pasaka
(Mk 14:12-21; Lk 22:7-14,21-23; Yh 13:21-30)
17Ilipofika siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wafuasi wake walimjia Yesu na kumwambia, “Tutaandaa kila kitu kwa ajili yako ili ule mlo wa Pasaka. Unataka tuandae wapi mlo wa Pasaka?”
18Yesu akajibu, “Nendeni mjini kwa mtu ninayemfahamu. Mwambieni kuwa Mwalimu anasema, ‘Muda uliowekwa kwa ajili yangu umekaribia sana. Mimi na wafuasi wangu tutakula mlo wa Pasaka katika nyumba yako.’” 19Walitii na kufanya kama Yesu alivyowaambia. Waliandaa mlo wa Pasaka.
20Jioni ilipowadia, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. 21Walipokuwa wakila Yesu akasema, “Niaminini, ninapowaambia kuwa mmoja wenu ninyi kumi na wawili atanikabidhi kwa maadui zangu.”
22Wanafunzi walisikitika sana waliposikia hili. Kila mmoja akasema, “Bwana, hakika si mimi!”
23Yesu akajibu, “Yeye aliyechovya mkate wake katika kikombe kile kile nilichochovya mimi ndiye atakayenisaliti. 24Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama Maandiko yanavyosema. Lakini ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Adamu ili auawe. Ni bora mtu huyo asingezaliwa.”
25Ndipo Yuda, ambaye ndiye angemsaliti, akamwambia Yesu, “Mwalimu, hakika si mimi unayemzungumzia, ama ndiye?”
Yesu akamjibu, “hicho ndicho unachosema.”
Chakula cha Bwana
(Mk 14:22-26; Lk 22:15-20; 1 Kor 11:23-25)
26Walipokuwa wakila, Yesu alichukua baadhi ya mikate na akamshukuru Mungu. Alimega baadhi ya vipande, akawapa wafuasi wake na akasema, “Chukueni mkate huu na mle. Ni mwili wangu.”
27Kisha akachukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu na akawapa. Akasema, “Kila mmoja wenu anywe divai iliyo katika kikombe hiki. 28Divai hii ni damu yangu, itakayomwagika ili kusamehe dhambi za watu wengi na kuanza Agano Jipya ambalo Mungu analifanya na watu wake. 29Ninataka mjue kuwa, hii ni mara ya mwisho nitakunywa divai mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”
30Waliimba wimbo kwa pamoja kisha wakaenda kwenye Mlima wa Mizeituni.
Yesu Asema Petro Atamkana
(Mk 14:27-31; Lk 22:31-34; Yh 13:36-38)
31Yesu akawaambia wafuasi wake, “Usiku wa leo ninyi nyote mtapoteza imani yangu kwangu. Maandiko yanasema,
‘Nitamwua mchungaji,
na kondoo watatawanyika.’#Zek 13:7
32Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka Kisha nitakwenda Galilaya. Nitakuwa huko kabla ninyi hamjaenda huko.”
33Petro akajibu, “Wafuasi wengine wote wanaweza kupoteza imani juu yako. Lakini imani yangu haitatetereka.”
34Yesu akajibu, “Ukweli ni huu, usiku wa leo utasema haunifahamu. Utanikana mara tatu kabla jogoo hajawika.”
35Lakini Petro akajibu, “Sitasema kwamba sikufahamu! Mimi hata nitakufa pamoja nawe!” Na wafuasi wengine wote wakasema kitu hicho hicho.
Yesu Aomba Akiwa Peke Yake
(Mk 14:32-42; Lk 22:39-46)
36Kisha Yesu akaondoka pamoja na wafuasi wake na kwenda mahali panapoitwa Gethsemane. Akawaambia, “Kaeni hapa wakati ninakwenda mahali pale kuomba.” 37Alimwambia Petro na wana wawili wa Zebedayo waende pamoja naye. Kisha akaanza kuhuzunika na kuhangaika. 38Yesu akamwambia Petro na wana wa Zebedayo, “Moyo wangu ni mzito na wenye huzuni hata kujisikia kana kwamba huzuni hiyo itaniua. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.”
39Kisha Yesu akaenda mbele kidogo. Akainama hadi chini uso wake ukiigusa nchi akiomba na akasema, “Baba yangu, ikiwezekana, usifanye nikinywee kikombe hiki cha mateso.#26:39 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao. Lakini fanya lile ulitakalo na si lile ninalolitaka mimi.” 40Kisha akarudi walipokuwa wafuasi wake na akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Je hamkuwa na uwezo wa kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41Amkeni kesheni na kuomba ili muyashinde majaribu. Roho zenu zinataka kufanya mambo sahihi, lakini miili yenu ni dhaifu.”
42Kisha Yesu akaenda mara ya pili na akaomba akisema, “Baba yangu, ikiwa ni lazima nikinywee kikombe hiki na haiwezekani nikakwepa, basi mapenzi yako na yatimizwe.”
43Kisha akarudi na kwenda walipokuwa wafuasi wake, akawakuta wamelala tena. Hawakuweza kukesha. 44Hivyo akawaacha akaenda tena kuomba. Mara hii ya tatu alipokuwa anaomba akasema kama alivyosema hapo mwanzo.
45Kisha Yesu akawarudia wafuasi wake na akasema, “Bado mnalala na kupumzika? Wakati wa Mwana wa Adamu kukabidhiwa kwa wenye dhambi umewadia. 46Simameni! Tuondoke. Tazama yeye atakayenikabidhi anakuja.”
Yesu Akamatwa
(Mk 14:43-50; Lk 22:47-53; Yh 18:3-12)
47Yesu alipokuwa anazungumza, Yuda mmoja wa wanafunzi wake kumi na mbili alifika akiwa na kundi kubwa la watu, waliokuwa wamebeba majambia na marungu. Walikuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48Yuda aliyekuwa amkabidhi Yesu kwao, alipanga kufanya kitu cha kuwajulisha yupi kati ya wafuasi alikuwa Yesu. Alisema, “Mtu nitakayembusu ndiye mtakayemkamata.” 49Hivyo Yuda alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Salamu, Mwalimu!” Kisha akambusu.
50Yesu akajibu, “Rafiki yangu, fanya ulilokuja kufanya.”
Kisha wale watu wakaja na kumkamata Yesu. 51Jambo hili lilipotokea, mmoja wa wafuasi wa Yesu alichukua jambia lake na kumkata sikio mtumishi wa kuhani mkuu.
52Yesu akamwambia, “Rudisha jambia lako mahali pake. Atumiaye jambia atauawa kwa jambia. 53Hakika unajua kuwa ningemwomba Baba yangu yeye angenipa zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika. 54Lakini hilo lisingekubaliana na yale Maandiko, yanayosema hivi ndivyo ilivyopasa itokee.”
55Kisha Yesu akaliambia kundi, “Kwa nini mnakuja kunikamata mkiwa na mikuki na marungu kama vile mimi ni mhalifu? Nimekuwa nakaa eneo la Hekalu nikifundisha kila siku. Kwa nini hamkunikamata kule? 56Lakini mambo haya yote yametokea ili kutimiza Maandiko yaliyoandikwa na manabii.” Ndipo wafuasi wake wote wakamwacha na kukimbia.
Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini
(Mk 14:53-65; Lk 22:54-55,63-71; Yh 18:13-14,19-24)
57Wale waliomkamata Yesu wakampeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu. Walimu wa Sheria na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwa wamekusanyika huko. 58Petro alimfuata Yesu lakini alikuwa mbali kidogo. Alimfuata mpaka katika ua wa nyumba ya kuhani mkuu. Petro alienda uani na akakaa pamoja na walinzi. Alitaka kuona nini kingetokea.
59Viongozi wa makuhani na baraza kuu walijaribu kutafuta kosa ili waweze kumwua Yesu. Walijaribu kutafuta watu ili wadanganye kuwa Yesu alifanya kosa. 60Watu wengi walikuja na akasema uongo kuhusu Yesu. Lakini baraza lilishindwa kupata ushahidi wa kuutumia ili kumwua. Ndipo watu wawili walikuja 61na akasema, “Mtu huyu#26:61 Mtu huyu Yaani, Yesu. Adui zake walikuwa wanakwepa kutamka jina lake. alisema, ‘Ninaweza kuliharibu Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’”
62Kisha kuhani mkuu alisimama na kumwambia Yesu, “Huna neno lolote la kujitetea dhidi ya mashtaka haya juu yako? Wanasema kweli?” 63Lakini Yesu hakusema neno lolote.
Kisha kuhani mkuu akamwambia Yesu, “Apa mbele za Mungu aliye hai kwamba utatuambia kweli. Je! wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu?”
64Yesu akajibu, “Unaweza akasema hivyo, Mimi ndiye. Lakini ninawaambia, kitambo kidogo mtamwona Mwana wa Adamu akiwa amekaa upande wa kuume wa Mungu, mwenye Nguvu. Na mtamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
65Kuhani mkuu aliposikia hili, alilarua vazi lake kwa hasira. Akasema, “Mtu huyu amemtukana Mungu! Hatuhitaji mashahidi zaidi. Ninyi nyote mmesikia matusi yake. 66Mnasemaje?”
Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ana hatia, na ni lazima afe.”
67Na baadhi ya waliokuwa pale wakamtemea mate Yesu usoni na kumpiga makonde na wengine walimpiga makofi. 68Wakasema, “Tuonyeshe kuwa wewe ni nabii, Masihi! Nani amekupiga!”
Petro Amkana Yesu
(Mk 14:66-72; Lk 22:56-62; Yh 18:15-18,25-27)
69Petro alipokuwa amekaa nje uani, msichana mtumishi akamwendea. Akasema, “Ulikuwa pamoja na Yesu, yule mtu kutoka Galilaya.”
70Lakini Petro akamwambia kila mtu aliyekuwa pale kuwa si kweli. Akasema “Sijui unachosema.”
71Kisha akaondoka uani. Akiwa kwenye lango msichana mtumishi akamwona na akawaambia watu waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.”
72Kwa mara nyingine tena Petro akasema hakuwa pamoja na Yesu. Akasema, “Ninaapa kwa Mungu, simfahamu mtu huyu!”
73Baada ya muda mfupi baadaye, watu waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro na kumwambia, “Tunajua wewe ni mmoja wao. Hata namna unavyoongea inaonesha wazi kuwa ndivyo hivyo.”
74Kisha Petro akaanza kujiapiza mwenyewe ikiwa anaongopa. Akasema, “Ninaapa kwa Mungu, simfahamu mtu huyu!” Mara alipomaliza akasema hili, jogoo akawika. 75Kisha akakumbuka maneno alivyoambiwa na Yesu kuwa: “Kabla jogoo hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha Petro akatoka nje na kulia kwa uchungu sana.

S'ha seleccionat:

Mathayo 26: TKU

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió