Luka 18

18
Mfano wa mjane asiyekata tamaa
1Kisha Isa akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa. 2Akawaambia, “Katika mji mmoja palikuwa hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu. 3Katika mji huo alikuwako mjane mmoja aliyekuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’
4“Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Ijapokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu, 5lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’ ”
6Bwana Isa akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu. 7Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia? 8Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”
Mfano wa Farisayo na mtoza ushuru
9Isa akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10“Watu wawili walienda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyang’anyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’
13“Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’
14“Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”
Isa awabariki watoto wadogo
(Mathayo 19:13-15; Marko 10:13-16)
15Pia, watu walikuwa wakimletea Isa watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea. 16Lakini Isa akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. 17Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”
Mtawala tajiri
(Mathayo 19:16-30; Marko 10:17-31)
18Mtawala mmoja akamuuliza Isa, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
19Isa akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 20Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’#18:20 Kutoka 20:12-16; Kumbukumbu 5:16-20
21Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
22Isa aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
23Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi. 24Isa akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu! 25Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
26Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
27Isa akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.”
28Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”
29Isa akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu 30ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”
Isa atabiri tena kifo chake
(Mathayo 20:17-19; Marko 10:32-34)
31Isa akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa. 32Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua. 33Naye siku ya tatu atafufuka.”
34Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Isa alikuwa anazungumzia nini.
Isa amponya kipofu karibu na Yeriko
(Mathayo 20:29-34; Marko 10:46-52)
35Isa alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada. 36Kipofu huyo aliposikia umati wa watu wakipita, akauliza nini kilikuwa kikitendeka. 37Wakamwambia, “Isa Al-Nasiri anapita.”
38Akapaza sauti, akasema, “Isa, Mwana wa Daudi#18:38 Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4)., nihurumie!”
39Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea, wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
40Isa akasimama, akawaamuru wamlete huyo mtu kwake. Alipokaribia, Isa akamuuliza, 41“Unataka nikufanyie nini?”
Akajibu, “Bwana, nataka kuona.”
42Isa akamwambia, “Basi upate kuona. Imani yako imekuponya.” 43Akapata kuona mara hiyo, akamfuata Isa, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.

S'ha seleccionat:

Luka 18: NENO

Subratllat

Comparteix

Copia

None

Vols que els teus subratllats es desin a tots els teus dispositius? Registra't o inicia sessió