Λογότυπο YouVersion
Εικονίδιο αναζήτησης

Matendo 1

1
Waumini wa Isa wa kwanza
(Matendo 1:1–5:42)
Ahadi ya Roho wa Mungu
1Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, Theofilo, kuhusu mambo yote Isa aliyoyafanya na kufundisha tangu mwanzo, 2hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho Mtakatifu wa Mungu wale mitume aliowachagua. 3Baada ya mateso yake, alijionesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu ufalme wa Mungu. 4Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba#1:4 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu., ambayo mmenisikia nikisema habari zake. 5Yahya aliwabatiza#1:5 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. Wafuasi wa Isa Al-Masihi pia wanapokea Roho wa Mungu kama dhibitisho ya imani yao. kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho wa Mungu.”
Isa apaa mbinguni
(Marko 16:19-20; Luka 24:50-53)
6Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Isa, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
7Isa akawaambia, “Sio wajibu wenu kujua nyakati au majira ambayo Baba ameyaweka kwa mamlaka yake mwenyewe. 8Lakini mtapokea nguvu, Roho wa Mungu akiwajilia juu yenu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na Yudea yote, na Samaria, na miisho ya dunia.”
9Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
10Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake mbinguni, ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao. 11Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Isa aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni, atarudi tena jinsi hiyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.”
Mathiya achaguliwa nafasi ya Yuda
(Mathayo 27:3-10)
12Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato#1:12 kama kilomita moja kutoka mjini. 13Walipowasili mjini Yerusalemu, walienda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Waliokuwepo walikuwa:
Petro, Yohana, Yakobo na Andrea;
Filipo na Tomaso;
Bartholomayo na Mathayo,
Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote#1:13 Wazelote walikuwa kikundi cha Kiyahudi wenye imani kali waliompinga Kaisari na utawala wa Rumi. na Yuda mwana wa Yakobo.
14Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pia walikuwepo wanawake kadhaa, na Mariamu mama yake Isa, na ndugu zake Isa.
15Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao walikuwa watu wapatao mia moja na ishirini), akasema, 16“Ndugu zangu, ilibidi andiko litimie, ambalo Roho wa Mungu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda, aliyewaongoza wale waliomkamata Isa. 17Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”
18(Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje. 19Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu.)
20“Kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Zaburi,
“ ‘Mahali pake na pawe ukiwa,
wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’#1:20 Zaburi 69:25
na,
“ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’#1:20 Zaburi 109:8
21Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Isa alipokuwa akiishi kati yetu, 22kuanzia ubatizo wa Yahya hadi siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”
23Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yusufu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya. 24Kisha wakaomba, wakasema, “Mwenyezi Mungu, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuoneshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25ili achukue nafasi ya huduma ya utume, ambayo Yuda aliiacha ili aende anapostahili.” 26Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.

Επιλέχθηκαν προς το παρόν:

Matendo 1: NENO

Επισημάνσεις

Κοινοποίηση

Αντιγραφή

None

Θέλετε να αποθηκεύονται οι επισημάνσεις σας σε όλες τις συσκευές σας; Εγγραφείτε ή συνδεθείτε