3
Yahya na Isa, na kujaribiwa kwa Isa
(Luka 3:1–4:13)
Yahya atayarisha njia
(Mathayo 3:1-12; Marko 1:1-8; Yohana 1:19-28)
1Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Yudea, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania akiwa mfalme wa Abilene, 2nao Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, neno la Mungu likamjia Yahya, mwana wa Zakaria huko jangwani. 3Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi#3:3 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali.. 4Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:
“Sauti ya mtu aliaye nyikani,
‘Itengenezeni njia ya Mwenyezi Mungu,
yanyoosheni mapito yake.
5Kila bonde litajazwa,
kila mlima na kilima vitashushwa.
Njia zilizopinda zitanyooshwa,
na zilizoparuza zitasawazishwa.
6Nao watu wote watauona
wokovu wa Mungu.’#3:6 Isaya 40:3-5”
7Yahya akaambia umati ule wa watu waliokuwa wanakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? 8Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Ibrahimu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Ibrahimu watoto kutoka mawe haya. 9Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”
10Umati ule wa watu wakamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?”
11Yahya akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”
12Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Mwalimu na sisi inatupasa tufanyeje?”
13Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”
14Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?”
Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”
15Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yahya angeweza kuwa ndiye Al-Masihi#3:15 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.. 16Yahya akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji#3:16 au ndani ya maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho wa Mungu na kwa moto. 17Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” 18Basi, kwa maonyo mengine mengi Yahya aliwasihi na kuwahubiria watu Habari Njema.
19Lakini Yahya alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia, mke wa ndugu yake, na maovu mengine aliyokuwa amefanya, 20Herode aliongezea jambo hili kwa hayo mengine yote: alimfunga Yahya gerezani.
Isa abatizwa
(Mathayo 3:13-17; Marko 1:9-11)
21Baada ya watu wote kubatizwa, Isa naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka. 22Roho Mtakatifu wa Mungu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua, nayo sauti kutoka mbinguni ikasema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”
Ukoo wa Isa
(Mathayo 1:1-17)
23Isa alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yusufu.
Yusufu alikuwa mwana wa Eli,
24Eli alikuwa mwana wa Mathati,
Mathati alikuwa mwana wa Lawi,
Lawi alikuwa mwana wa Melki,
Melki alikuwa mwana wa Yana,
Yana alikuwa mwana wa Yusufu,
25Yusufu alikuwa mwana wa Matathia,
Matathia alikuwa mwana wa Amosi,
Amosi alikuwa mwana wa Nahumu,
Nahumu alikuwa mwana wa Esli,
Esli alikuwa mwana wa Nagai,
26Nagai alikuwa mwana wa Maathi,
Maathi alikuwa mwana wa Matathia,
Matathia alikuwa mwana wa Semei,
Semei alikuwa mwana wa Yoseki,
Yoseki alikuwa mwana wa Yoda,
27Yoda alikuwa mwana wa Yoanani,
Yoanani alikuwa mwana wa Resa,
Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli,
Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli,
Shealtieli alikuwa mwana wa Neri,
28Neri alikuwa mwana wa Melki,
Melki alikuwa mwana wa Adi,
Adi alikuwa mwana wa Kosamu,
Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu,
Elmadamu alikuwa mwana wa Eri,
29Eri alikuwa mwana wa Yoshua,
Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri,
Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu,
Yorimu alikuwa mwana wa Mathati,
Mathati alikuwa mwana wa Lawi,
30Lawi alikuwa mwana wa Simeoni,
Simeoni alikuwa mwana wa Yuda,
Yuda alikuwa mwana wa Yusufu,
Yusufu alikuwa mwana wa Yonamu,
Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu,
Eliakimu alikuwa mwana wa Melea,
31Melea alikuwa mwana wa Mena,
Mena alikuwa mwana wa Matatha,
Matatha alikuwa mwana wa Nathani,
Nathani alikuwa mwana wa Daudi,
32Daudi alikuwa mwana wa Yese,
Yese alikuwa mwana wa Obedi,
Obedi alikuwa mwana wa Boazi,
Boazi alikuwa mwana wa Salmoni,
Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni,
33Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu,
Aminadabu alikuwa mwana wa Aramu,
Aramu alikuwa mwana wa Esromu,
Esromu alikuwa mwana wa Peresi,
Peresi alikuwa mwana wa Yuda,
34Yuda alikuwa mwana wa Yakobo,
Yakobo alikuwa mwana wa Isaka,
Isaka alikuwa mwana wa Ibrahimu,
Ibrahimu alikuwa mwana wa Tera,
Tera alikuwa mwana wa Nahori,
35Nahori alikuwa mwana wa Serugi,
Serugi alikuwa mwana wa Ragau,
Ragau alikuwa mwana wa Pelegi,
Pelegi alikuwa mwana wa Eberi,
Eberi alikuwa mwana wa Sala,
36Sala alikuwa mwana wa Kenani,
Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi,
Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu,
Shemu alikuwa mwana wa Nuhu,
Nuhu alikuwa mwana wa Lameki,
37Lameki alikuwa mwana wa Methusela,
Methusela alikuwa mwana wa Idrisi,
Idrisi alikuwa mwana wa Yaredi,
Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli,
Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani,
38Kenani alikuwa mwana wa Enoshi,
Enoshi alikuwa mwana wa Sethi,
Sethi alikuwa mwana wa Adamu,
Adamu alikuwa mwana wa Mungu#3:38 Yaani mwana wa kiroho, bali si wa kimwili. Adamu aliumbwa moja kwa moja kutoka kwake Mwenyezi Mungu mwenyewe..