UTANGULIZI
Kabla ya utangulizi wenyewe juu ya kitabu hiki, inafaa kusema machache ambayo yanahusu vitabu vitano vya kwanza vya Biblia ambavyo katika utamaduni wa kidini wa Wayahudi vilijulikana kwa jina moja: “Torah” jina lenye maana ya Sheria au Mwongozo. Tazama pia Utangulizi wa Agano la Kale. Wayahudi waliozungumza lugha ya Kigiriki waliviita vitabu hivyo vyote vitano “Pentateuko” yaani “Kitabu katika sehemu tano.” Vitabu hivyo vinajulikana pia kama Vitabu vya Mose, na tafsiri nyingine huvitaja kama Kitabu cha kwanza cha Mose (Mwanzo), Kitabu cha pili cha Mose (Kutoka) n.k. Basi ufuatao ni utangulizi mfupi juu ya kitabu hiki cha “Mwanzo.”
Neno “Mwanzo” (Kitabu cha Mwanzo) linamaanisha: Chimbuko, chanzo, asili; nalo linatumiwa kukitaja kitabu hiki cha kwanza cha Agano la Kale kwani chenyewe kinasimulia hasa juu ya jinsi ulimwengu ulivyoanza kuwako, asili au chimbuko la binadamu na asili ya Waisraeli.
Kitabu cha Mwanzo chaweza kugawanyika katika sehemu mbili kuu:
Sura 1–11: Historia ya awali ya kale juu ya ulimwengu na binadamu. Simulizi hili linatokana na imani thabiti kwamba ulimwengu wote uliumbwa na Mungu na kwamba watu walitokana na wazazi wa kwanza walioumbwa na Mungu, kwamba uovu, mateso na kifo duniani chanzo chake ni watu wenyewe.
Baada ya historia hiyo ya awali ya kale tunasimuliwa jinsi Mungu alivyowaadhibu watu kwa gharika kuu na jinsi Noa alivyookolewa katika maangamizi hayo. Kisha tunafahamishwa juu ya asili ya mataifa na lugha tofauti katika simulizi la Mnara wa Babeli (Sura 11.)
Sura 12–50: Historia ya kale ya Waisraeli. Mungu alijichagulia watu wa Israeli ili kwa kupitia kwao mataifa mengine yamjue Mungu na kubarikiwa. Kwa hiyo, Mungu alimwita Abrahamu (12:1–25:18) ambaye anasifika kwa imani yake na utii wake kwa Mungu, kisha mwanawe wa pili, yaani Isaka, halafu Yakobo (25:19–37:1) ambaye alipewa jina ambalo limekuwa jina la taifa hilo Mungu alilochagua – Israeli. Yakobo alikuwa na wanawe kumi na wawili ambao walikuwa chanzo cha makabila kumi na mawili ya Israeli. Mmoja wao, Yosefu, (37:2–50:28) alikuwa babu wa makabila mawili: Efraimu na Manase.
Kitovu cha masimulizi hayo yote katika kitabu hiki cha Mwanzo ni Mwenyezi-Mungu mwenyewe: Mwanzoni tunaambiwa kuwa yeye ndiye aliyeumba mbingu na dunia (yaani kila kitu) na kwamba tangu mwanzo ameahidi kuujalia ulimwengu baraka zake, na kitabu kinaishia kwa kurudia tena kwamba Mungu ataendelea kuwajalia binadamu baraka zake. Masimulizi hayo yamekusanywa pamoja kutokana na imani thabiti juu ya Mungu Muumba wa vitu vyote.