Mwanzo 2

2
1 Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.
2 Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. 3 Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.
Adamu Na Eva
4 Haya ndiyo maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa.
Bwana Mungu alipoziumba mbingu na dunia, 5 hapakuwepo na mche wa shambani uliokuwa umejitokeza ardhini, wala hapakuwepo na mmea wa shamba uliokuwa umeota, kwa kuwa Bwana Mungu alikuwa hajanyeshea mvua juu ya nchi, na hapakuwepo mtu wa kuilima ardhi, 6lakini umande ulitokeza kutoka ardhini na kunyesha uso wote wa nchi: 7 Bwana Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi#2:7 Neno la Kiebrania la mavumbi ya ardhi ndilo kiini cha jina Adamu. ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai.
8 Basi Bwana Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemuumba. 9 Bwana Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Katikati ya bustani ulikuwepo mti wa uzima na mti wa kujua mema na mabaya.
10 Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni, kuanzia hapa ukagawanyika kuwa mito minne. 11 Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu. 12 (Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri, bedola na vito shohamu pia hupatikana huko.) 13Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi. 14 Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki ya Ashuru. Mto wa nne ni Frati.
15 Bwana Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza. 16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani, 17 lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”
18 Bwana Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”
19 Basi Bwana Mungu alikuwa amefanyiza kutoka ardhi wanyama wote wa porini na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa ndilo jina lake. 20 Hivyo Adamu akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, ndege wa angani, na wanyama wote wa porini.
Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa. 21 Hivyo Bwana Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. 22 Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.
23 Huyo mwanaume akasema,
“Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu
na nyama ya nyama yangu,
ataitwa ‘mwanamke,’#2:23 Jina la Kiebrania la mwanamke linafanana na lile la mwanaume.
kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”
24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
25 Adamu na mkewe wote wawili walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.

נבחרו כעת:

Mwanzo 2: NEN

הדגשה

שתף

העתק

None

רוצים לשמור את ההדגשות שלכם בכל המכשירים שלכם? הירשמו או היכנסו