Matendo 1

1
Jumuiya ya Waumini wa Kwanza
(1:1–5:42)
Ahadi Ya Roho Wa Mwenyezi Mungu
1 Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, mpendwa Theofilo, kuhusu mambo yote Isa aliyofanya na kufundisha tangu mwanzo, 2 hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho wa Mwenyezi Mungu wale mitume aliowachagua. 3 Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mwenyezi Mungu. 4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba,#1:4 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. ambayo mmenisikia nikisema habari zake. 5 Yahya aliwabatiza#1:5 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. Wafuasi wa Isa Al-Masihi pia wanapokea Roho wa Mwenyezi Mungu kama dhibitisho ya imani yao. kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho wa Mwenyezi Mungu.”
Isa Apaa Mbinguni
(Marko 16:19-20; Luka 24:50-53)
6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Isa, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
7 Isa akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho wa Mwenyezi Mungu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, 11 wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Isa aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”
Mathiya Achaguliwa Badala Ya Yuda
(Mathayo 27:3-10)
12 Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato#1:12 Mwendo wa Sabato hapa ina maana umbali wa mita 1,100. kutoka mjini. 13 Walipowasili mjini Yerusalemu, walikwenda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Wale waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Tomaso, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote#1:13 Zelote hapa ina maana alikuwa mwanachama wa Wazelote, kikundi cha Kiyahudi cha kupinga jeuri ya Warumi. na Yuda mwana wa Yakobo. 14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Mariamu mama yake Isa, pamoja na ndugu zake Isa.
15 Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema, 16 “Ndugu zangu, ilibidi Andiko litimie ambalo Roho wa Mwenyezi Mungu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Isa. 17 Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”
18 (Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje. 19 Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu).
20 “Kama vile ilivyoandikwa katika kitabu cha Zaburi,
“ ‘Mahali pake na pawe ukiwa,
wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’
na,
“ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’
21 Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Isa alipoingia na kutoka katikati yenu, 22 kuanzia ubatizo wa Yahya mpaka siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”
23 Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yusufu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya. 24 Kisha wakaomba, wakasema, “Mwenyezi Mungu, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25 ili achukue nafasi ya huduma ya utume ambayo Yuda aliiacha ili aende mahali pake mwenyewe.” 26 Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.

Jelenleg kiválasztva:

Matendo 1: NMM

Kiemelés

Megosztás

Másolás

None

Szeretnéd, hogy a kiemeléseid minden eszközödön megjelenjenek? Regisztrálj vagy jelentkezz be