2
Arusi Huko Kana
1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Isa alikuwepo pale. 2Isa pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia. 3Divai ilipokwisha, mama yake Isa akamwambia, “Wameishiwa na divai.”
4 Isa akamwambia, “Mwanamke, nina nini nawe? Saa yangu haijawadia.”
5 Mama yake akawaambia wale watumishi, “Lolote atakalowaambia, fanyeni.”
6 Basi ilikuwepo mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu.#2:6 Kipipa kimoja chenye ujazo wa lita 40; hivyo kila mtungi ulikuwa na ujazo wa lita 80 au 120.
7Isa akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu.
8Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.”
Hivyo wakachota, wakampelekea. 9 Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando 10akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.”
11 Huu, ndio uliokuwa muujiza wa kwanza Isa aliofanya Kana ya Galilaya. Hivyo Isa alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
Isa Atakasa Hekalu
(Mathayo 21:12-13; Marko 11:15-17; Luka 19:45-46)
12Baada ya hayo, Isa pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka mpaka Kapernaumu, wakakaa huko siku chache.
13 Ilipokaribia wakati wa Pasaka#2:13 Sherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri. ya Wayahudi, Isa alipanda kwenda Yerusalemu. 14 Huko Hekaluni#2:14 Nyumba kuu ya ibada kwa Waisraeli iliyokuwa Yerusalemu. aliwakuta watu wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha. 15Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka kwenye eneo la Hekalu, pamoja na kondoo na ng’ombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao. 16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba#2:16 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu kuwa mahali pa biashara?”
17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”
18 Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya?”
19 Isa akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”
20Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?” 21 Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Isa aliyokuwa amesema.
23 Ikawa Isa alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, wakaamini katika jina lake. 24Lakini Isa hakujiaminisha kwao kwa sababu aliwajua wanadamu wote. 25 Hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote kuhusu mtu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa mtu.