Logo YouVersion
Icona Cerca

Yohana MT. 1

1
1MWANZO alikuwako Neno, nae Neno alikuwako kwa Mungu, nae Neno alikuwa Mungu. 2Huyu mwanzo alikuwako kwa Mungu. 3Vyote vyalifanyika kwa huyu. Wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. 4Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao uzima ulikuwa nuru ya watu, 5nayo nuru yangʼaa gizani, wala giza halikuiweza. 6Palitokea mtu ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7Huyu alikuja kwa ushuhuda, illi aishuhudie nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. 8Huyu hakuwa ile nuru, illakini aishuhudie ile nuru. 9Kulikuwako nuru halisi, imtiayo nuru killa mtu ajae katika ulimwengu. 10Alikuwako ulimwenguni, ulimwengu umepata kuwa kwa veye, wala ulimwengu haukumtambua. 11Alikuja kwake, nao walio wake hawakumpokea. 12Bali wote waliompokea aliwapa mamlaka ya kufanyika watoto wa Mungu, ndio waliaminio jina lake: 13waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. 14Nae Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, tukautazama utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee akitoka kwa Baba, amejaa neema na kweli. 15Yohana akamshuhudia, akapaaza sauti yake, akinena, Huyu ndiye niliyemnena khabari zake, kwamba, Ajae nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. 16Na katika ujazi wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. 17Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa, neema na kweli zilikuwa kwa mkono wa Yesu Kristo. 18Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote, Mwana wa pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyefasiri khabari yake.
19Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma makuhani na Walawi toka Yerusalemi wamwulize, Wewe u nani? 20Nae aliungama wala hakukana; aliungama, Mimi siye Kristo. 21Wakamwuliza, Nini bassi? U Eliya wewe? Akanena, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. 22Bassi wakamwambia, U nani? tuwape majibu waliotupeleka. Wajinenaje? 23Akasema, Mimi ni sauti ya mtu apaazae sauti jangwani, Inyosheni njia ya Bwana! kama alivyonena nabii Isaya. 24Nao waliotumwa walitoka kwa Mafarisayo. 25Wakamwuliza, wakimwambia, Mbona bassi wabatiza, kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? 26Yohana akawajibu akanena, Mimi nabatiza kwa maji: kati mwenu amesimama msiyemjua ninyi. 27Ndiye ajae nyuma yangu, aliyekuwa mbele yangu, wala mimi sistahili niilegeze gidam ya kiatu chake. 28Haya yalifanyika Bethania ngʼambu ya Yardani, alikokuwako Yohana akibatiza.
29Siku ya pili yake Yohana amwona Yesu anakuja kwake, akanena, Tazama, Mwana Kondoo wa Mungu, aichukuae dhambi ya ulimwengu! 30Huyu ndiye niliyemnena khabari zake, Yuaja mtu nyuma yangu, aliyekuwa mbele yangu, kwa maana alikuwa kabla yangu. 31Nami sikumjua: lakini kusudi adhibirishwe kwa Israeli ndio maana nalikuja nikibatiza kwa maji. 32Yohana akashuhudu, akasema, Nimemwona Roho akishuka, kama hua, kutoka mbinguni; akakaa juu yake. 33Nami sikumjua, lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyu aliniambia, Yeye ambae utakaemwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyu ndiye abatizae kwa Roho Mtakatifu. 34Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.
35Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa amesimama na wawili katika wanafunzi wake. 36Akamtazama Yesu, akitembea, akasema, Tazama, Mwana Kondoo wa Mungu! 37Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu. Yesu akageuka, akawaona wakifuata: akawaambia, Mnatafuta nini? 38Wakamwambia, Rabbi (tafsiri yake, Mwalimu), unakaa wapi? Akawaambia, Njoni muone. 39Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Ilikuwa karibu na saa kumi. 40Andrea, ndugu ya Simon Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana na kumfuata. 41Huyu akamwona kwanza Simon, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi, (tafsiri yake Kristo). 42Akampeleka kwa Yesu. Yesu akamtazama, akasema, Wewe Simon, mwana wa Yona, utakwitwa Kefa (tafsiri yake, Petro).
43Siku ya pili yake Yesu akataka kuondoka kwenda Galilaya, akamwona Filipo, akamwambia, Nifuate. 44Nae Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mtu wa mji wa Andrea na Petro.
45Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na na manabii, Yesu, mwana wa Yusuf, mtu wa Nazareti 46Nathanaeli akamwambia, Chaweza kitu chema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone. 47Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake, akamtaja khabari zake, Tazama, huyu ni Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. 48Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunijua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwa chini ya mtini, nalikuona. 49Nathanaeli akajibu, akamwambia, Rabbi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe mfalme wa Israeli. 50Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nalikuambla, Nalikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. 51Akamwambia, Amin, amin, nakuambieni, Tangu sasa mtaziona mbingu zimefunguka, na malaika wa Mungu wakipanda, wakishuka juu ya Mwana wa Adamu.

Attualmente Selezionati:

Yohana MT. 1: SWZZB1921

Evidenziazioni

Condividi

Copia

None

Vuoi avere le tue evidenziazioni salvate su tutti i tuoi dispositivi?Iscriviti o accedi