Mwanzo 1
1
Siku sita za uumbaji
1Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.
3Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. 4Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema; ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. 5Mungu akaiita nuru “mchana”, na giza akaliita “usiku”. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.
6Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji, igawe maji na maji.” 7Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. 8Mungu akaiita hiyo nafasi “anga”. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.
9Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10Mungu akaiita nchi kavu “ardhi”, nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.
11Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. 13Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.
14Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, 15nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17Mungu akaiweka hiyo mianga katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.
20Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21Kwa hiyo Mungu akaumba wanyama wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” 23Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.
24Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: mifugo, viumbe vinavyotambaa ardhini na wanyama pori, kila kiumbe kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, mifugo kulingana na aina zake, na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
26Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini na ndege wa angani, na mifugo na wanyama pori wote, na dunia yote, na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini.”
27Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,
kwa mfano wa Mungu alimuumba;
mwanaume na mwanamke aliwaumba.
28Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”
29Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30Nao wanyama wote wa nchi, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.
31Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, vilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.
Atualmente Selecionado:
Mwanzo 1: NENO
Destaque
Compartilhar
Copiar
Quer salvar seus destaques em todos os seus dispositivos? Cadastre-se ou faça o login
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.