1 Nyakati 17:16-27
1 Nyakati 17:16-27 NENO
Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za BWANA, akasema: “Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? Kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Mungu, umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Umeniangalia kama mtu aliyetukuka kuliko watu wote, Ee BWANA Mungu. “Daudi aweza kukuambia nini zaidi kuhusu kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe unamjua mtumishi wako, Ee BWANA Mungu. Kwa ajili ya mtumishi wako, tena sawasawa na mapenzi yako, umefanya jambo hili kuu na kujulisha ahadi hizi zote zilizo kuu sana. “Hakuna aliye kama wewe, Ee BWANA Mungu, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe. Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli: taifa pekee duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya maajabu makubwa na ya kutisha, kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? Uliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee BWANA Mungu, umekuwa Mungu wao. “Basi sasa, Ee BWANA, ahadi uliyoweka kuhusu mtumishi wako na nyumba yake, na uithibitishe milele. Fanya kama ulivyoahidi, ili ithibitike na jina lako litakuwa kuu milele. Kisha watu watasema, ‘BWANA wa majeshi, Mungu aliye juu ya Israeli, ndiye Mungu wa Israeli.’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itafanywa imara mbele zako. “Wewe, Mungu wangu, umemfunulia mtumishi wako Daudi kwamba utamjengea nyumba. Hivyo mtumishi wako amekuwa na ujasiri wa kukuomba maombi haya. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu! Umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. Basi imekupendeza kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu milele machoni pako; kwa ajili yako, Ee BWANA, umeibariki, nayo itabarikiwa milele.”