5
Imani katika Mwana wa Mwenyezi Mungu huushinda ulimwengu
1Kila mtu anayeamini kwamba Isa ndiye Al-Masihi amezaliwa#5:1 Kiroho, sio kwa njia ya kimwili. na Mungu, na yeyote ampendaye Baba humpenda pia mtoto aliyezaliwa naye. 2Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake. 3Huku ndiko kumpenda Mungu, yaani kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito. 4Kwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, yaani hiyo imani yetu. 5Ni nani yule aushindaye ulimwengu? Ni yule tu aaminiye kwamba Isa ni Mwana wa Mungu#5:5 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili..
Ushuhuda kuhusu Mwana wa Mwenyezi Mungu
6Huyu ndiye alikuja kwa maji na damu, yaani Isa Al-Masihi. Hakuja kwa maji peke yake, bali kwa maji na damu. Naye Roho wa Mungu ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli. 7Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni: hao ni Baba, Neno na Roho wa Mungu. Hawa watatu ni umoja. 8Pia wako mashahidi watatu duniani]#5:7-8 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.: hao ni Roho, Maji na Damu; hawa watatu wanakubaliana katika umoja. 9Kama tunaukubali ushuhuda wa wanadamu, basi ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi, kwa kuwa huu ndio ushuhuda wa Mungu kwamba amemshuhudia Mwanawe. 10Kila mtu amwaminiye Mwana wa Mungu anao huu ushuhuda moyoni mwake. Kila mtu asiyemwamini Mungu amemfanya yeye kuwa mwongo, kwa sababu hakuamini ushuhuda Mungu alioutoa kuhusu Mwanawe. 11Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupatia uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe. 12Aliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima.
Maneno ya mwisho
13Nawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele. 14Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. 15Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.
16Mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo. Ninamaanisha wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo. 17Jambo lolote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.
18Tunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hawezi kumdhuru. 19Sisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu. 20Nasi pia twajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupatia sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani ndani ya Isa Al-Masihi Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.
21Watoto wapendwa, jilindeni nafsi zenu kutokana na sanamu. Amen.