1 Wafalme 1:38-53
1 Wafalme 1:38-53 NENO
Hivyo kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi wakaenda na kumpandisha Sulemani juu ya nyumbu wa Mfalme Daudi, nao wakamsindikiza hadi Gihoni. Kuhani Sadoki akachukua pembe ya mafuta kutoka hema takatifu na kumtia Sulemani mafuta. Kisha wakapiga tarumbeta na watu wote wakapaza sauti wakisema, “Mfalme Sulemani aishi maisha marefu!” Na watu wote wakakwea wakimfuata, huku wakipiga filimbi na kushangilia sana, hata ardhi ikatikisika kwa ile sauti. Adoniya pamoja na wageni wote waliokuwa pamoja naye wakasikia sauti hiyo walipokuwa wakimalizia karamu yao. Waliposikia sauti ya tarumbeta, Yoabu akauliza, “Nini maana ya makelele haya yote katika mji?” Hata alipokuwa anaongea, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akafika. Adoniya akasema, “Ingia ndani. Mtu wa maana kama wewe ni lazima awe amelete habari njema.” Yonathani akamjibu, “La hasha! Mfalme Daudi bwana wetu amemfanya Sulemani kuwa mfalme. Mfalme ametuma pamoja naye kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, nao kuhani Sadoki na nabii Nathani wamempaka mafuta huko Gihoni kuwa mfalme. Kutoka hapo wamepanda wakishangilia, na sauti zimeenea kote katika mji. Hizo ndizo kelele unazosikia. Zaidi ya hayo, Sulemani ameketi kwenye kiti chake cha ufalme. Pia, maafisa wa mfalme wamekuja ili kumpongeza bwana wetu Mfalme Daudi, wakisema, ‘Mungu wako na alifanye jina la Sulemani kuwa mashuhuri kuliko lako, na kiti chake cha ufalme kiwe na ukuu kuliko chako!’ Naye mfalme akasujudu akiabudu kitandani mwake, akasema, ‘Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye ameruhusu macho yangu kuona mrithi kwenye kiti changu cha ufalme leo.’ ” Waliposikia haya, wageni wote wa Adoniya wakainuka kwa hofu na kutawanyika. Lakini Adoniya kwa kumwogopa Sulemani, akaenda na kushika pembe za madhabahu. Kisha Sulemani akaambiwa, “Adoniya anamwogopa Mfalme Sulemani na ameshikilia pembe za madhabahu. Anasema, ‘Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hatamuua mtumishi wake kwa upanga.’ ” Sulemani akajibu, “Akijionesha kuwa mtu muungwana, hakuna unywele wake utakaoanguka juu ya ardhi; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa.” Ndipo Mfalme Sulemani akawatuma watu, nao wakamshusha kutoka madhabahuni. Naye Adoniya akaja akamwinamia Mfalme Sulemani, naye Sulemani akamwambia, “Nenda nyumbani mwako.”