1 Wafalme 15:1-8
1 Wafalme 15:1-8 NENO
Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya akawa mfalme wa Yuda, naye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka binti Abishalomu. Alitenda dhambi zote baba yake alizotenda kabla yake; moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake ulivyokuwa. Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi, Mwenyezi Mungu, Mungu wake, akampa taa katika Yerusalemu kwa kumwinua mwana atawale baada yake ili kuifanya Yerusalemu kuwa imara. Kwa kuwa Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, wala hakushindwa kuzishika amri zote za Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yake, isipokuwa kwa suala la Uria, Mhiti. Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu wakati wote wa maisha ya Abiya. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Abiya na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu. Naye Abiya akalala na baba zake akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake.