1 Wafalme 2:1-11
1 Wafalme 2:1-11 NENO
Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Sulemani agizo. Akasema, “Ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jioneshe kuwa mwanaume, shika lile Mwenyezi Mungu, Mungu wako, analokuagiza: Nenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote utakapoenda, na ili Mwenyezi Mungu aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’ “Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake. Mtendee kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani. “Lakini uwaoneshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu. “Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, aliyenilaani kwa laana kali siku niliyoenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwa Mwenyezi Mungu: ‘Sitakuua kwa upanga!’ Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.” Kisha Daudi akalala na baba zake, naye akazikwa katika Mji wa Daudi. Daudi alikuwa ametawala Israeli miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na tatu.