1
Kuzaliwa kwa Samweli
1Kulikuwa na mtu mmoja kutoka Rama, Msufi kutoka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyeitwa Elkana mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu Mwefraimu. 2Alikuwa na wake wawili; mmoja aliitwa Hana na mwingine Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na mtoto.
3Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani wa Mwenyezi Mungu. 4Kila mara ilipofika siku ya Elkana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote wa kiume na wa kike. 5Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunga tumbo. 6Kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi. 7Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipoenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha hadi analia na kushindwa kula. 8Elkana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”
9Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la Mwenyezi Mungu. 10Kwa uchungu wake mwingi Hana alimwomba Mwenyezi Mungu, akilia kwa uchungu. 11Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa Mwenyezi Mungu kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.”
12Alipokuwa anaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu, Eli alichunguza kinywa chake. 13Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa 14naye akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achilia mbali mvinyo wako.”
15Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa Mwenyezi Mungu. 16Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa kutokana na uchungu mkuu na huzuni.”
17Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.”
18Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena.
19Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za Mwenyezi Mungu na kisha wakarudi nyumbani mwao huko Rama. Elkana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye Mwenyezi Mungu akamkumbuka. 20Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina Samweli, akisema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa Mwenyezi Mungu.”
Hana amweka Samweli wakfu
21Huyo mtu Elkana alipopanda pamoja na jamaa yake yote kutoa dhabihu ya mwaka kwa Mwenyezi Mungu na kutimiza nadhiri yake, 22Hana hakuenda. Alimwambia mume wake, “Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, nitamchukua na kumpeleka mbele za Mwenyezi Mungu, naye ataishi huko daima.”
23Elkana mumewe akamwambia, “Fanya lile unaloona ni bora zaidi kwako. Ukae hapa hadi utakapomwachisha kunyonya, Mwenyezi Mungu na akujalie kutimiza nadhiri yako.” Hivyo huyo mwanamke akakaa nyumbani na kumnyonyesha mwanawe hadi alipomwachisha kunyonya.
24Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, Hana akamchukua huyo mtoto, akiwa mdogo hivyo hivyo, pamoja na fahali wa miaka mitatu, efa ya unga#1:24 Efa moja ya unga ni sawa na kilo 22. na kiriba cha divai, naye akamleta mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Shilo. 25Walipokwisha kumchinja yule fahali, wakamleta mtoto kwa Eli, 26naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwa Mwenyezi Mungu. 27Niliomba mtoto huyu, naye Mwenyezi Mungu amenijalia kile nilichomwomba. 28Hivyo sasa ninamtoa kwa Mwenyezi Mungu. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa Mwenyezi Mungu.” Naye akamwabudu Mwenyezi Mungu huko.