Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 11

11
Sauli aukomboa mji wa Yabeshi
1Nahashi Mwamoni akakwea kuuzingira mji wa Yabesh-Gileadi kwa jeshi. Wanaume wote wa Yabeshi wakamwambia, “Fanya mkataba nasi, na tutakutumikia.”
2Lakini Nahashi yule Mwamoni akajibu, “Nitafanya mkataba na ninyi tu kwa sharti kwamba nitang’oa jicho la kulia la kila mmoja wenu, na hivyo kuleta aibu juu ya Israeli yote.”
3Viongozi wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe siku saba ili tuweze kutuma wajumbe katika Israeli yote. Ikies hakuna hata mmoja atayekuja kutuokoa, tutajisalimisha kwako.”
4Wajumbe walipofika Gibea ya Sauli na kutoa taarifa kuhusu masharti haya kwa watu, wote walilia kwa sauti kubwa. 5Wakati huo huo Sauli alikuwa anarudi kutoka mashambani, akiwa nyuma ya maksai wake, naye akauliza, “Watu wana nini? Mbona wanalia?” Ndipo wakamweleza vile wanaume wa Yabeshi walivyokuwa wamesema.
6Sauli aliposikia maneno yao, Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akawaka hasira. 7Akachukua maksai wawili na kuwakata vipande vipande, naye kuvituma hivyo vipande kupitia wajumbe katika Israeli yote, wakitangaza, “Hivi ndivyo itakavyofanyika kwa maksai wa kila mmoja ambaye hatamfuata Sauli na Samweli.” Kisha kicho cha Mwenyezi Mungu kikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja. 8Sauli alipowakusanya huko Bezeki, wanaume wa Israeli walikuwa elfu mia tatu, na wanaume wa Yuda elfu thelathini.
9Wakawaambia wale wajumbe waliokuwa wamekuja, “Waambieni wanaume wa Yabesh-Gileadi, ‘Kesho kabla jua halijawa kali, mtaokolewa.’ ” Wajumbe walipoenda na kutoa taarifa hii kwa wanaume wa Yabeshi, wakafurahi. 10Wakawaambia Waamoni, “Kesho tutajisalimisha kwenu, nanyi mtaweza kututendea chochote mnachoona chema kwenu.”
11Kesho yake Sauli alitenganisha watu wake katika vikosi vitatu; wakati wa zamu ya mwisho ya usiku wakaingia katika kambi ya Waamoni na kuwachinja hadi mchana. Wale walionusurika wakatawanyika, hivi kwamba hawakusalia watu wawili pamoja.
Sauli athibitishwa kuwa mfalme
12Kisha watu wakamwambia Samweli, “Ni nani yule aliyeuliza, ‘Je, Sauli atatutawala?’ Tuletee hawa watu, nasi tutawaua.”
13Lakini Sauli akasema, “Hakuna hata mmoja atakayeuawa leo, kwa kuwa siku hii Mwenyezi Mungu ameokoa Israeli.”
14Ndipo Samweli akawaambia watu, “Njooni, twendeni Gilgali na huko tuthibitishe ufalme.” 15Kwa hiyo watu wote wakaenda Gilgali na kumthibitisha Sauli kuwa mfalme mbele za Mwenyezi Mungu. Huko wakatoa dhabihu za sadaka za amani mbele za Mwenyezi Mungu, naye Sauli na Waisraeli wote wakafanya karamu kubwa.

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 11: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia