Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 9

9
Wasaidieni wafuasi wa Al-Masihi wenzenu
1Hakuna haja ya kuwaandikia kuhusu huduma hii kwa watakatifu. 2Kwa kuwa ninajua mlivyo na shauku ya kusaidia, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili ya jambo hilo kwa Wamakedonia, nikiwaambia kwamba ninyi watu wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana. Na shauku yenu imewachochea wengi wao katika kutoa. 3Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusiwe maneno matupu, bali mpate kuwa tayari kama nilivyosema mngekuwa tayari. 4Kwa maana nikija na Mmakedonia yeyote na kuwakuta hamko tayari, sisi, na hata ninyi pia, tungeona haya kwa kuwa na ujasiri hivi katika ninyi. 5Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kwenu kabla yangu, wafanye mipango ya hayo matoleo ya ukarimu mliyokuwa mmeahidi, ili yawe tayari kama matoleo ya hiari wala si kama ya kutozwa kwa nguvu.
Kupanda kwa ukarimu
6Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye haba pia atavuna haba, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9Kama ilivyoandikwa:
“Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini;
haki yake hudumu milele.”#9:9 Zaburi 112:9
10Yeye ampaye mpanzi mbegu ya kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.
12Huduma hii mnayofanya si tu ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi kwake Mungu. 13Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Al-Masihi, na kwa ukarimu wenu wa kuwashirikisha wao na watu wengine wote. 14Nayo mioyo yao itawaonea shauku wanapowaombea, kwa sababu ya neema ipitayo kiasi mliyopewa na Mungu. 15Mungu apewe shukrani kwa karama yake isiyoelezeka!

Iliyochaguliwa sasa

2 Wakorintho 9: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia