19
Yoabu amkemea mfalme
1Yoabu akaambiwa, “Mfalme analia na kumwombolezea Absalomu.” 2Kwa jeshi lote, ushindi wa siku ile ukageuka kuwa maombolezo, kwa sababu siku ile vikosi vilisikia ikisemwa, “Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.” 3Siku ile watu wakaingia mjini kimya kama vile waingiavyo kwa aibu watu waliokimbia kutoka vitani. 4Mfalme akafunika uso wake akalia kwa sauti, akisema, “Ee mwanangu Absalomu! Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”
5Kisha Yoabu akaingia ndani ya nyumba ya mfalme na kusema, “Leo umewaaibisha watu wako wote, waliookoa maisha yako, maisha ya wanao wa kiume na wa kike, maisha ya wake zako na masuria wako. 6Unawapenda wale wanaokuchukia, na unawachukia wale wanaokupenda. Leo umeonesha wazi kwamba majemadari wako na watu wao hawana maana kwako. Naona kwamba ungefurahi kama Absalomu angekuwa hai leo na sisi sote tuwe tumekufa. 7Sasa utoke nje ukawatie moyo watu wako. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba ikiwa hutatoka nje, hakuna mtu atakayesalia pamoja nawe ifikapo leo jioni. Hii itakuwa mbaya zaidi kwako kuliko maafa yote yaliyokupata tangu ujana wako hadi sasa.”
8Kwa hiyo, mfalme akaondoka na kuketi kwenye kiti chake langoni. Watu walipoambiwa, “Mfalme ameketi langoni,” watu wote wakamjia.
Daudi arudi Yerusalemu
Wakati huo, Waisraeli walikuwa wamekimbilia nyumbani mwao. 9Katika makabila yote ya Israeli, watu walikuwa wanabishana wao kwa wao, wakisema, “Mfalme alituokoa kutoka mikononi mwa adui zetu; ndiye alituokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti. Lakini sasa mfalme ameikimbia nchi kwa sababu ya Absalomu, 10naye Absalomu, tuliyempaka mafuta atutawale, amekufa vitani. Basi mbona hamsemi lolote kuhusu kumrudisha mfalme?”
11Mfalme Daudi akapeleka ujumbe huu kwa makuhani Sadoki na Abiathari, kusema: “Waulizeni wazee wa Yuda, ‘Kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme katika jumba lake la kifalme, maadamu kile kinachosemwa katika Israeli yote kimemfikia mfalme katika makao yake? 12Ninyi ni ndugu zangu, mwili wangu na damu yangu mwenyewe. Kwa hiyo kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme?’ 13Nanyi mwambieni Amasa, ‘Je, wewe si mwili wangu mwenyewe na damu yangu? Mungu na aniadhibu vikali zaidi, kama kuanzia sasa na kuendelea wewe si jemadari wa jeshi langu mahali pa Yoabu.’ ”
14Alivutia mioyo ya watu wote wa Yuda, kama vile walikuwa mtu mmoja. Wakapeleka ujumbe kwa mfalme, kusema, “Rudi, wewe na watumishi wako wote.” 15Ndipo mfalme akarudi, akaenda hadi kufikia Mto Yordani.
Basi watu wa Yuda walikuwa wamekuja Gilgali ili kutoka kwenda kumlaki mfalme na kumvusha Mto Yordani. 16Shimei mwana wa Gera, wa kabila la Benyamini kutoka Bahurimu, akaharakisha kuteremka pamoja na wanaume wa Yuda ili kumlaki Mfalme Daudi. 17Pamoja naye walikuwa Wabenyamini elfu moja wakiwa wamefuatana na Siba, msimamizi wa nyumba ya Sauli, pia wanawe kumi na watano, na watumishi ishirini. Wakaharakisha kwenda Yordani, mahali mfalme alipokuwa. 18Wakavuka kivuko ili kuwachukua watu wa nyumbani mwa mfalme ili kuwavusha na kufanya kila kitu alichotaka.
Shimei mwana wa Gera alipovuka Yordani, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme, 19na kumwambia, “Bwana wangu na asinihesabie hatia. Usikumbuke jinsi mtumishi wako alivyofanya kosa siku ile bwana wangu mfalme alipoondoka Yerusalemu. Mfalme aliondoe moyoni mwake. 20Kwa maana mimi mtumishi wako najua nimefanya dhambi, lakini leo nimekuja hapa kama wa kwanza wa nyumba yote ya Yusufu kushuka na kumlaki bwana wangu mfalme.”
21Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, Shimei hapaswi kuuawa kwa ajili ya hili? Alimlaani mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.”
22Daudi akajibu, “Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya? Siku ya leo mmekuwa adui zangu! Je, leo kuna yeyote atakayeuawa katika Israeli? Je, mimi sijui kuwa leo ndimi mfalme katika Israeli yote?” 23Basi mfalme akamwambia Shimei, “Hutakufa.” Naye mfalme akamwahidi kwa kiapo.
24Pia Mefiboshethi mwana wa Sauli akashuka kwenda kumlaki mfalme. Hakuwa amenawa miguu, wala kunyoa ndevu zake, wala kufua nguo zake tangu siku mfalme alipoondoka Yerusalemu hadi siku aliporudi salama. 25Alipotoka Yerusalemu kuja kumlaki mfalme, basi mfalme akamuuliza, “Mefiboshethi, kwa nini hukufuatana nami?”
26Akasema, “Bwana wangu mfalme, maadamu mimi mtumishi wako ni kiwete, nilisema, ‘Nitandikiwe punda wangu, nimpande, ili niweze kwenda pamoja na mfalme.’ Lakini Siba mtumishi wangu akanisaliti. 27Naye amemchongea mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme. Bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu, kwa hiyo fanya lolote linalokupendeza. 28Wazao wote wa baba yangu hawastahili kitu kingine isipokuwa kifo kutoka kwa bwana wangu mfalme, lakini ulimpa mtumishi wako nafasi miongoni mwa wale waliokula mezani pako. Je, ninayo haki gani kumwomba mfalme zaidi ya hayo?”
29Mfalme akamwambia, “Kwa nini useme zaidi? Naamuru wewe na Siba mgawanye mashamba.”
30Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu achukue kila kitu, kwa kuwa sasa bwana wangu mfalme amerudi nyumbani salama.”
31Barzilai, Mgileadi, pia akashuka kutoka Rogelimu ili kuvuka Yordani pamoja na mfalme na kumsindikiza kutoka huko. 32Basi Barzilai alikuwa mzee sana mwenye umri wa miaka themanini. Alikuwa amempatia mfalme mahitaji alipokuwa anaishi huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa mtu tajiri sana. 33Mfalme akamwambia Barzilai, “Vuka pamoja nami na ukae nami huko Yerusalemu, nami nitakupatia mahitaji yako.”
34Lakini Barzilai akamjibu mfalme, “Je, nitaishi miaka mingine mingapi, hata nipande kwenda Yerusalemu pamoja na mfalme? 35Sasa nina miaka themanini. Je, naweza kutofautisha kati ya lililo jema na lililo baya? Je, mtumishi wako anaweza kujua ladha ya kile anachokula au anachokunywa? Je, bado naweza kusikiliza sauti za waimbaji wa kiume na za wanawake? Kwa nini mtumishi wako aongeze mzigo kwa bwana wangu mfalme? 36Mtumishi wako atavuka Yordani pamoja na mfalme kwa umbali mfupi tu, lakini kwa nini mfalme anizawadie kwa namna hii? 37Mruhusu mtumishi wako arudi, ili mimi nikafie katika mji wangu mwenyewe karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini yupo hapa mtumishi wako Kimhamu. Mruhusu avuke pamoja na bwana wangu mfalme. Mtendee lolote linalokupendeza.”
38Mfalme akamwambia Barzilai, “Kimhamu atavuka Yordani pamoja nami, nami nitamtendea lolote litakalokupendeza. Nawe kitu chochote unachotaka kutoka kwangu nitakutendea.”
39Kwa hiyo watu wote wakavuka Yordani, kisha mfalme akavuka. Mfalme akambusu Barzilai na kumbariki; Barzilai akarudi nyumbani mwake.
40Mfalme alipovuka kwenda Gilgali, Kimhamu akavuka pamoja naye. Vikosi vyote vya Yuda na nusu ya vikosi vya Israeli vilimvusha mfalme.
41Baada ya kitambo kidogo, wanaume wote wa Israeli wakaja kwa mfalme na kumwambia, “Kwa nini ndugu zetu, wanaume wa Yuda, wamemrudisha mfalme kwa siri bila kutushirikisha, na kumvusha ng’ambo ya Yordani, yeye na nyumba yake, pamoja na watu wake wote?”
42Wanaume wote wa Yuda wakawajibu wanaume wa Israeli, “Tulifanya hivi kwa sababu mfalme ni jamaa yetu wa karibu. Kwa nini mnakasirikia jambo hili? Je, tumekula kitu chochote cha mfalme? Je, tumejichukulia kitu chochote kwa ajili yetu wenyewe?”
43Ndipo wanaume wa Israeli wakawajibu wanaume wa Yuda, “Tunayo haki mara kumi kwa mfalme; sisi tunahusika zaidi na Daudi kuliko ninyi. Kwa nini basi mnatudharau? Je, hatukuwa wa kwanza kuzungumza kuhusu kumrudisha mfalme nyumbani?”
Lakini wanaume wa Yuda wakajibu kwa ukali hata kuliko wanaume wa Israeli.