2 Samweli 7:18-29
2 Samweli 7:18-29 NEN
Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za BWANA, akasema: “Ee BWANA Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo? Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee BWANA Mwenyezi, wewe umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee BWANA Mwenyezi? “Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, Ee BWANA Mwenyezi. Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako. “Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee BWANA Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe, Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee BWANA, umekuwa Mungu wao. “Basi sasa, BWANA, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Fanya kama ulivyoahidi, ili kwamba jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘BWANA Mwenye Nguvu Zote ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako. “Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hii. Ee BWANA Mwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu mbele zako milele, kwa maana wewe, Ee BWANA Mwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”