Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 24

24
Mbele ya Feliksi huko Kaisaria
1Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania akateremka hadi Kaisaria pamoja na baadhi ya wazee na mwanasheria aitwaye Tertulo, wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala. 2Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na mabadiliko mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele. 3Wakati wote na kila mahali, kwa namna yoyote, mtukufu Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi. 4Lakini nisije nikakuchosha zaidi, ningekuomba kwa hisani yako utusikilize kwa kifupi.
5“Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanasiri, 6na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata. [Tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu. 7Lakini jemadari Lisia alitujia na nguvu nyingi, akamwondoa mikononi mwetu, 8akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako.]#24:6-8 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. Kwa kumchunguza mwenyewe utaweza kujua ukweli kuhusu mashtaka haya yote tunayoleta dhidi yake.”
9Pia wale Wayahudi wakaunga mkono wakithibitisha kuwa mashtaka haya yote ni kweli.
Paulo ajitetea mbele ya Feliksi
10Mtawala Feliksi alipompungia Paulo mkono ili ajitetee, yeye akajibu, “Najua kwamba wewe umekuwa hakimu katika taifa hili kwa miaka mingi, hivyo natoa utetezi wangu kwa furaha. 11Unaweza kuhakikisha kwa urahisi kuwa hazijapita zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu kuabudu. 12Hawa wanaonishtaki hawakunikuta nikibishana na mtu yeyote Hekaluni au kuchochea umati wa watu katika sinagogi#24:12 Nyumba ya ibada na mafunzo. au mahali pengine popote mjini. 13Wala hawawezi kabisa kukuthibitishia mashtaka haya wanayoleta dhidi yangu. 14Lakini ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu kama mfuasi wa Njia Ile, ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Torati na kile kilichoandikwa katika Manabii, 15nami ninalo tumaini kwa Mungu, ambalo hata wao wenyewe wanalikubali kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, kwa wenye haki na wasio na haki. 16Kwa hiyo ninajitahidi siku zote kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu na mbele za wanadamu.
17“Basi, baada ya miaka mingi nilikuja Yerusalemu ili kuwaletea watu wangu msaada kwa ajili ya maskini na kutoa dhabihu. 18Nilikuwa nimetakaswa waliponikuta Hekaluni nikifanya mambo haya. Hapakuwa na umati wa watu pamoja nami, wala sikuhusika katika ghasia yoyote. 19Lakini kuna Wayahudi fulani kutoka jimbo la Asia ambao walipaswa kuwa hapa mbele yako na kunishtaki kama wana jambo lolote dhidi yangu. 20Au, watu hawa walio hapa waseme ni kosa gani walilonipata nalo waliponisimamisha mbele ya Baraza la Wayahudi#24:20 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu., 21isipokuwa ni kuhusu jambo hili moja nililopaza sauti mbele yao na kusema, ‘Mimi nashtakiwa mbele yenu leo kwa sababu ya ufufuo wa wafu.’ ”
22Basi Feliksi, ambaye alifahamu vizuri habari za Njia Ile#24:22 Njia Ile maana yake wafuasi wa Isa (Yohana 14:6; Matendo 24:14); walichukuliwa kuwa dhehebu la dini ya Wayahudi., akaahirisha kesi ile, akasema, “Jemadari Lisia atakapoteremka huku, nitaamua kesi yenu.” 23Ndipo akaamuru kiongozi wa askari amweke chini ya ulinzi lakini ampe uhuru na kuwaruhusu rafiki zake wamhudumie.
24Baada ya siku kadhaa, Feliksi alikuja pamoja na Drusila mkewe, aliyekuwa Myahudi. Alituma aitiwe Paulo, naye akamsikiliza alipokuwa akinena kuhusu imani katika Al-Masihi Isa. 25Naye Paulo alipokuwa akinena kuhusu haki, kuwa na kiasi na kuhusu hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu, akasema, “Hiyo yatosha sasa! Unaweza kuondoka. Nitakapokuwa na muda, nitakuita.” 26Wakati huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempa rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye.
27Baada ya miaka miwili kupita, Porkio Festo akaingia kwenye utawala mahali pa Feliksi, lakini kwa kuwa Feliksi alitaka kuwapendeza Wayahudi, akamwacha Paulo gerezani.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 24: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia