Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 3:1-10

Matendo 3:1-10 NEN

Siku moja Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali yapata saa tisa alasiri. Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni. Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka. Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.” Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu. Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu, wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia.