Matendo 4:23-37
Matendo 4:23-37 NENO
Punde Petro na Yohana walipoachiliwa, walirudi kwa waumini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee. Watu waliposikia hayo, wakapaza sauti zao, wakamwomba Mungu kwa pamoja, wakisema, “Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeziumba mbingu na nchi na bahari, na vitu vyote vilivyomo. Wewe ulinena kwa Roho wa Mungu kupitia kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ukasema: “ ‘Mbona mataifa wanaghadhibika, na makabila ya watu kuwaza ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, na watawala wanakusanyika pamoja dhidi ya Mwenyezi Mungu na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.’ Ni kweli Herode na Pontio Pilato, pamoja na watu wa Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu kupanga njama dhidi ya mwanao mtakatifu Isa, uliyempaka mafuta. Wakafanya yale uweza wako na mapenzi yako yalikusudia yatokee tangu zamani. Sasa, Mwenyezi Mungu, angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu. Nyoosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Isa.” Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Waumini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Isa kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. Wala hapakuwa mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. Yusufu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.