Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 5:12-21

Matendo 5:12-21 NENO

Mitume walifanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Waumini wote walikuwa wakikusanyika katika Ukumbi wa Sulemani. Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao, ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. Hata hivyo, waliomwamini Bwana Isa wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake. Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa. Kisha kuhani mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye, waliokuwa wa kundi la Masadukayo, wakajawa na wivu. Wakawakamata mitume na kuwafunga gerezani. Lakini wakati wa usiku, malaika wa Mwenyezi Mungu akaja, akafungua milango ya gereza na akawatoa nje. Akawaambia, “Nendeni, mkasimame Hekaluni, mkawaambie watu maneno yote ya maisha haya mapya.” Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu. Kuhani mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya Baraza la Wayahudi, yaani wazee wote wa Israeli. Wakatumana wale mitume waletwe kutoka gerezani.