Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amosi 1:1-10

Amosi 1:1-10 NEN

Maneno ya Amosi, mmoja wa wachunga wanyama wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli. Alisema: “BWANA ananguruma toka Sayuni, pia ananguruma kutoka Yerusalemu; malisho ya wachunga wanyama yanakauka, kilele cha Karmeli kinanyauka.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Dameski, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliipura Gileadi kwa vyombo vya chuma vyenye meno. Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi. Nitalivunja lango la Dameski; nitamwangamiza mfalme aliyeko katika Bonde la Aveni, na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni. Watu wote wa Aramu watakwenda uhamishoni huko Kiri,” asema BWANA. Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Gaza, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu walichukua mateka jumuiya nzima na kuwauza kwa Edomu, nitatuma moto juu ya kuta za Gaza ambao utateketeza ngome zake. Nitamwangamiza mfalme wa Ashdodi na yeye aishikaye fimbo ya utawala katika Ashkeloni. Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni, hadi Mfilisti wa mwisho atakapokufa,” asema BWANA Mwenyezi. Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Tiro, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu ameuza jumuiya nzima ya mateka kwa Edomu, na kutokujali mapatano ya undugu, Nitatuma moto kwenye kuta za Tiro ambao utateketeza ngome zake.”