Amosi 4:4-13
Amosi 4:4-13 NEN
“Nendeni Betheli mkatende dhambi; nendeni Gilgali mkazidi kutenda dhambi. Leteni dhabihu zenu kila asubuhi, zaka zenu kila mwaka wa tatu. Mchome mkate uliotiwa chachu kama sadaka ya shukrani, jisifuni kuhusu sadaka zenu za hiari: jigambeni kwa ajili ya sadaka hizo, enyi Waisraeli, kwa kuwa hili ndilo mnalopenda kulitenda,” asema BWANA Mwenyezi. “Niliwapa njaa kwenye kila mji, na ukosefu wa chakula katika kila mji, hata hivyo bado hamjanirudia mimi,” asema BWANA. “Pia niliwazuilia ninyi mvua miezi mitatu kabla ya kufikia mavuno. Nilinyesha mvua kwenye mji mmoja, lakini niliizuia mvua isinyeshe mji mwingine. Shamba moja lilipata mvua, na lingine halikupata, nalo likakauka. Watu walitangatanga mji hata mji kutafuta maji, lakini hawakupata ya kuwatosha kunywa, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema BWANA. “Mara nyingi nilizipiga bustani zenu na mashamba ya mizabibu, niliyapiga kwa kutu na ukungu. Nzige walitafuna tini zenu na miti ya mizeituni, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema BWANA. “Niliwapelekea tauni miongoni mwenu kama nilivyofanya kule Misri. Niliwaua vijana wenu wa kiume kwa upanga, niliwachukua farasi wenu. Nilijaza pua zenu kwa uvundo kutoka kwenye kambi zenu, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema BWANA. “Niliwaangamiza baadhi yenu kama nilivyoangamiza Sodoma na Gomora. Mlikuwa kama kijiti kiwakacho kilichonyakuliwa motoni, hata hivyo hamjanirudia,” asema BWANA. “Kwa hiyo hili ndilo nitakalowafanyia, Israeli, na kwa sababu nitawafanyia hili, jiandaeni kukutana na Mungu wenu, ee Israeli.” Yeye ambaye hufanya milima, anaumba upepo, na kufunua mawazo yake kwa mwanadamu, yeye ageuzaye asubuhi kuwa giza, na kukanyaga mahali pa juu pa nchi: BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.