Amosi 5:18-27
Amosi 5:18-27 NEN
Ole wenu ninyi mnaoitamani siku ya BWANA! Kwa nini mnaitamani siku ya BWANA? Siku hiyo itakuwa giza, si nuru. Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba kumbe akakutana na dubu, kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta, kumbe akaumwa na nyoka. Je, siku ya BWANA haitakuwa giza, na si nuru: giza nene, bila mwonzi wa mwanga? “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini; siwezi kuvumilia makusanyiko yenu. Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka, sitazikubali. Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani, sitazitambua. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu! Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu. Lakini acheni haki itiririke kama mto, na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka! “Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli? Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu, Sikuthi mungu wenu mtawala, na Kiuni mungu wenu wa nyota, ambao mliwatengeneza wenyewe. Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,” asema BWANA, ambaye jina lake ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.