Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 7

7
Ndoto ya Danieli ya wanyama wanne
1Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Belshaza mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, nayo maono yakapita mawazoni mwake alipokuwa amelala kitandani mwake. Akayaandika mambo aliyoyaona katika ndoto yake.
2Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, na hapo mbele yangu kulikuwa na pepo kutoka pande nne za mbingu, zikivuruga bahari kuu. 3Wanyama wanne wakubwa, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka bahari.
4“Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa ya tai. Nikatazama hadi mabawa yake yalipong’olewa, naye akainuliwa katika nchi, akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.
5“Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, aliyefanana na dubu. Upande wake mmoja alikuwa ameinuka, na alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama, ushibe!’
6“Baada ya huyo, nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala.
7“Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya, tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma; akapondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chini ya nyayo zake chochote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi.
8“Nilipokuwa nikifikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ndogo, iliyojitokeza miongoni mwa zile kumi; pembe tatu za mwanzoni ziling’olewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu, na mdomo ulionena kwa majivuno.
9“Nilipoendelea kutazama,
“viti vya utawala vikawekwa,
naye Mzee wa Siku akaketi.
Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji;
nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama sufu.
Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka miali ya moto,
nayo magurudumu yake yote yalikuwa yanawaka moto.
10Mto wa moto ulikuwa unatiririka,
ukipita mbele yake.
Maelfu elfu wakamhudumia;
kumi elfu mara kumi elfu wakasimama mbele zake.
Mahakama ikakaa kuhukumu,
na vitabu vikafunguliwa.
11“Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia hadi yule mnyama alipouawa, na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto uliowaka. 12(Wanyama wengine walikuwa wamevuliwa mamlaka yao, lakini waliruhusiwa kuishi kwa muda.)
13“Katika maono yangu ya usiku nilitazama, na mbele yangu nikamwona mtu kama Mwana wa Adamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku, na akaongozwa mbele zake. 14Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu; nao watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.
Tafsiri ya ndoto ya hao wanyama
15“Mimi Danieli nilipata mahangaiko rohoni, nayo maono yale yaliyopita ndani ya mawazo yangu yalinisumbua. 16Nikamkaribia mmoja wa wale waliosimama pale, nikamuuliza maana halisi ya haya yote.
“Basi akaniambia na kunipa tafsiri ya vitu hivi: 17‘Hao wanyama wanne wakubwa ni falme nne zitakazoinuka duniani. 18Lakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele: naam, milele na milele.’
19“Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, aliyekuwa tofauti na wale wengine wote, tena wa kutisha sana, na meno yake ya chuma na makucha ya shaba: mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chochote kilichosalia. 20Pia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake, na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho kuliko zile nyingine, na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno. 21Nilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda, 22hadi huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipoumiliki ufalme.
23“Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote, nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda. 24Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu. 25Atanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwatesa watakatifu wake, huku akijaribu kubadili majira na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati#7:25 au chini ya mamlaka yake kwa mwaka mmoja, miaka miwili, na nusu mwaka.
26“ ‘Lakini mahakama itakaa kuhukumu, nayo mamlaka yake yataondolewa na kuangamizwa kabisa milele. 27Ndipo ufalme, mamlaka na ukuu wa falme chini ya mbingu yote zitakabidhiwa kwa watakatifu, watu wa Yeye Aliye Juu Sana. Ufalme wake utakuwa ufalme wa milele, nao watawala wote watamwabudu na kumtii yeye.’
28“Huu ndio mwisho wa jambo lile. Mimi Danieli nilitaabika sana katika mawazo yangu, nao uso wangu ukabadilika, lakini nililiweka jambo hilo moyoni mwangu.”

Iliyochaguliwa sasa

Danieli 7: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia