Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 29:1-13

Kumbukumbu 29:1-13 NEN

Haya ndiyo maneno ya Agano BWANA aliyomwagiza Mose kufanya na Waisraeli huko Moabu, kuwa nyongeza ya Agano alilofanya nao huko Horebu. Mose akawaita Waisraeli wote akawaambia: Macho yenu yameona yale yote BWANA aliyofanya kwa Mfalme Farao huko Misri, kwa maafisa wake wote na kwa nchi yake yote. Kwa macho yenu wenyewe mliona yale majaribu makubwa, ishara zile za miujiza na maajabu makubwa. Lakini mpaka leo BWANA hajawapa akili ya kuelewa au macho yanayoona au masikio yanayosikia. Kwa muda wa miaka arobaini niliyowaongoza jangwani, nguo zenu hazikuchakaa, wala viatu miguuni mwenu. Hamkula mkate na hamkunywa divai wala kileo chochote. Nilifanya hivi ili mpate kujua kuwa mimi ndimi BWANA Mungu wenu. Wakati mlipofika mahali hapa, Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani walikuja kupigana dhidi yetu, lakini tuliwashinda. Tuliichukua nchi yao na kuwapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kama urithi wao. Fuateni kwa bidii masharti ya Agano hili, ili kwamba mweze kustawi katika kila kitu mnachofanya. Ninyi nyote leo mnasimama mbele za BWANA Mungu wenu; mkiwa viongozi na wakuu wenu, wazee na maafisa wenu, na wanaume wengine wote wa Israeli, pamoja na watoto wenu, wake zenu na pia wageni waishio katika kambi zenu wanaowapasulia kuni na kuwachotea maji. Mnasimama hapa ili kufanya Agano na BWANA Mungu wenu, Agano ambalo Mungu analifanya nanyi siku hii ya leo na kulitia muhuri kwa kiapo, kuwathibitisha ninyi siku hii ya leo kama taifa lake, ili aweze kuwa Mungu wenu kama alivyowaahidi na kama alivyowaapia baba zenu Abrahamu, Isaki na Yakobo.